• HABARI MPYA

  Jumamosi, Julai 27, 2019

  KAGERE AFUNGA SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA TOWNSHIP ROLLERS LEO RUSTERNBURG

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Simba SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Township Rollers katika mchezo wa kirafiki uliofanyika leo asubuhi mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere alianza kuifungia Simba SC dakika ya 58 kabla ya kiungo wa kimataifa wa Botswana, Phenyo Nicolas Serameng kuisawazishia Township Rolleres dakika ya 70.
  Huo ulikuwa mchezo wa tatu wa kujipima nguvu kwa Simba SC katika kambi yake ya Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya, baada ya awali kushinda mechi mbili mfululizo.  
  Mabingwa hao wa Tanzania Bara walianza kwa kuifunga 4-0 timu ya Chuo Kikuu cha Orbit Tvet, kabla ya kuwachapa wenyeji, Platinums Stars FC 4-1, mechi zote zikipigwa mjini Rusternburg.

  Kwenye mechi na Orbit Tvet, mabao ya Simba SC yalifungwa na Nahodha na mshambuliaji tegemeo, John Raphael Bocco dakika ya tisa na 28, kiungo Hassan Dilunga dakika ya 23 na mshambuliaji mpya, Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino ya Daraja la Nne kwao, Brazil dakika ya 30.
  Dhidi ya Platinums Stars, Mzambia, Clatous Chama leo alifunga mabao mawili dakika za 11 na 58, wakati mabao mengine yalifungwa na viungo wenzake, Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman kwa penalti dakika ya 13 na Muzamil Yassin dakika ya 87, wakati la wenyeji lilifungwa na Ruele Modise dakika ya 75 kwa penalti pia.
  Baada ya mchezo wa leo, Simba itateremka tena uwanjani Jumanne kumenyana na Orlando Pirates ya Johannesburg kabla ya kurejea nyumbani kwa ajili ya tamasha la Simba Day Agosti 6 siku ambayo watamenyana na Power Dynamos ya Zambia Uwanja mjini Dar es Salaam katika mchezo mwingine wa kirafiki.
  Simba SC imelazimika kurudisha nyuma kwa siku mbili tamasha hilo ambalo kila mwaka hufanyika Agosti 8 baada ya ratiba ya Ligi Mabingwa Afrika kutoka ikionyesha mechi za kwanza za raundi ya Kwanza zitachezwa kati ya Agosti 9 na 11. 
  Simba SC wataanzia ugenini dhidi ya UD do Songo ya Msumbiji kati ya Agosti 9 na 11 kabla ya kurejea nyumbani kwa mchezo wa marudiano kati ya Agosti 23 na 25.
  Ikifanikiwa kuvuka raundi ya kwanza, Simba itakutana na mshindi kati ya FC Platinum ya Zimbabwe na Nyasa Bullets ya Malawi na ikifuzu mtihani huo pia itaingia tena hatua ya makundi.
  Wakati Simba ni mabingwa wa Bara, Power Dynamos walimaliza nafasi ya sita kwenye Kundi B Ligi Kuu ya Zambia msimu uliopita, ambalo Green Eagles iliongoza na kuingia fainali na kufungwa kwa penalti 3-1 na ZESCO United walioibuka mabingwa wa Zambia baada ya sare ya 0-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAGERE AFUNGA SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA TOWNSHIP ROLLERS LEO RUSTERNBURG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top