• HABARI MPYA

    Sunday, July 28, 2019

    TAIFA STARS YAJIWEKA PAGUMU KUFUZU CHAN 2020 BAADA YA SARE YA 0-0 NYUMBANI NA KENYA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TANZANIA imeshindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya kulazimishwa suluhu na Kenya katika mchezo wa kuwania tiketi ya fainali za michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN 2020 nchini Cameroon.
    Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Taifa Stars licha ya kupata nafasi kadhaa za kufunga, ilishindwa kuzifumania nyavu za Harambee Stars.
    Matokeo hayo yanaiweka Taifa Stars katika nafasi ngumu zaidi ya kucheza raundi ya mwisho ya kufuzu michuano hiyo ambayo huhusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, kwani itakuwa na mlima mrefu wa kupanda katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Agosti 4 Kasarani, Nairobi, Kenya.


    Katika kipindi cha kwanza, Taifa Stars walicheza vizuri na kulishambulia lango la wapinzani wao mara kadhaa, lakini kutokuwa makini kwa washambuliaji wake kulisababisha timu hiyo kushindwa kuibuka na ushindi mbele ya mashabiki wake.
    Kwa upande mwingine, Taifa Stars imeshindwa kulipa kisasi mbele ya Kenya baada ya kufungwa 3-2 katika mchezo wa hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019) nchini Misri.
    Hivyo, Taifa Stars inahitaji sare yoyote ya mabao au ushindi wa aina yoyote ili isonge mbele katika raundi ya mwisho, ambako itakutana na timu ya taifa ya Sudan na endapo ikipata ushindi wa jumla, itakata tiketi ya kwenda Cameroon, ambako fainali za Chan 2020 zitafanyikia.
    Taifa Stars kwa mara ya mwisho ilicheza fainali za CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast, ambazo ndizo zilikuwa za kwanza kufanyika tangu zilipoanzishwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
    Mchezo wa marudiano wa timu hizo utafanyika Nairobi, Kenya wikiend ijayo kwenye Uwanja wa Moi Kasarani.
    Kocha wa Taifa Stars baada ya kuona hakuna bao alimuingiza Ibrahi Ajibu aliyeanzia benchi na baadae Kelvin John waliochukua nafasi ya Ayub Lyanga na Hassan Dilunga, ambao angalau walionesha uhai kidogo, lakini Stars iliendelea kushindwa kufunga.
    Endapo mchezo wa marudiano utamalizika kwa suluhu, basi ushindi utaamliwa kwa mikwaju ya penalti ili kupata timu itakayocheza dhidi ya Sudan katika raundi ya mwisho ya kufuzu.
    Wapenzi wa soka nchini wameonekana kukatishwa tamaa na Stars, baada ya kushindwa kuwafuta machozi wapenzi hao wa soka baada ya kufanya vibaya Afcon 2019 kwa kufungwa mechi zote tatu za hatua ya makundi.
    Katika jaribio la mwisho, Aiyee nusura aipatie Stars bao baada ya kuachia mkwaju mkali wa mbali uliomshinda mlinda mlango wa Harambee Stars na kutoka nje kidogo ya lango.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Juma Kaseja, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/Kelvin John dk67, Salum Abubakar, John Bocco/Salim Aiyee dk85, Ayubu Lyanga/Ibrahim Ajibu dk54 na Idd Suleiman ‘Nado’.
    Kenya: John Oyemba, Bernard Ochieng, Mike Kibwage, Joash Onyango, Cliffton Miheso, Dennis Odhiambo, Kenneth Muguna, Musa Masika, Whyvonne Isuza, Duke Abuya na Enosh Ochieng.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAJIWEKA PAGUMU KUFUZU CHAN 2020 BAADA YA SARE YA 0-0 NYUMBANI NA KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top