• HABARI MPYA

  Ijumaa, Julai 12, 2019

  NUSU AFCON 2019; NI ALGERIA NA NIGERIA, SENEGAL NA TUNISIA

  TIMU za Algeria na Tunisa zimefanikiwa kwenda hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 baada ya ushindi kwenye mechi zao za Alhamisi usiku.
  Ilianza Algeria kuitoa Ivory Coast kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa New Suez kabla ya Tunisia kuinyuka Madagascar 3-0 Uwanja wa Al Salam mjini Cairo.
  Uwanja wa New Suez kiungo wa Galatasaray ya Uturuki, Sofiane Feghouli alianza kuifungia Algeria dakika ya 20, kabla ya mshambuliaji wa Aston Villa, Jonathan Kodjia kuisawazishia Ivory Coast dakika ya 62.
  Awali ya hapo, mshambuliaji Baghdad Bounedjah wa Al Sadd ya Qatar aliikosesha bao la pili Algeria baada ya kukosa penalty iliyogonga nguzo dakika ya 48.
  Mshambuliaji wa Manchester City, Riyad Mahrez aliiongoza Algeria kama Nahodha hadi dakika ya 86 alipotoka, wakati wa Wilfried Zaha wa Crystal Palace aliiongoza safu ya ushambuliaji ya Ivory Coast hadi dakika ya 94 alipompisha Gnaly Maxwell Cornet wa Lyon ya Ufaransa.
  Katika mikwaju ya penalti, shuti la Wilfried Bony liliokolewa na kipa wakati Geoffroy Serey Die aligongesha mwamba, huku Kessie, Cornet na Gradel pekee wakifunga.
  Waliofunga penalti za Algeria ni Bensebaini, Slimani, Delort, Ounas na Belaili na sasa timu hiyo itakutana na Nigeria katika Nusu Fainali Jumatatu Uwanja wa Kimataifa wa Cairo.
  Na Uwanja wa Al Salam mjini Cairo mabao ya kiungo wa Zamalek, Ferjani Sassi dakika ya 52, mshambuliaji wa AS Eupen ya Ubelgiji, Msakni Youssef dakika ya 60 na kiungo wa Dijon ya Ufaransa, Naim Sliti dakika ya 90 na ushei yakaivusha Algria dhidi ya Madagascar.
  Nusu Fainali zitachezwa Jumapili Senegal na Tunisia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Kimataifa wa Cairo kabla ya Algeria kupepetana na Nigeria Saa 4:00 usiku Uwanja wa JUni 30 mjini Cairo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NUSU AFCON 2019; NI ALGERIA NA NIGERIA, SENEGAL NA TUNISIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top