• HABARI MPYA

    Sunday, January 03, 2016

    HAJIB AITWA MAZEMBE KUZIBA PENGO LA SAMATTA…CHANONGO TAYARI YUKO LUBUMBASHI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Ibrahim Hajib Migomba anatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda kwenda Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kufanya majaribio ya kujiunga na klabu ya TP Mazembe ya huko.
    Mazembe kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kuwauza washambuliaji wake wawili, Watanzania, Mbwana Ally Samatta anayetakiwa na Genk ya Ubelgiji na Thomas Emmanuel Ulimwengu anayetakiwa na klabu za Ufaransa na Uturuki.
    Na katika kujiandaa na maisha bila wakali wake hao wa mabao waliotoa mchango mkubwa timu ikibeba taji la tano la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Mazembe inasaka nyota wengine chipukizi.
    Ibrahim Hajib anatarajiwa kwenda TP Mazembe wiki ijayo kufanya majaribio 

    Meneja wa Samatta, Jama Kisongo ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba mipango ya Hajib kwenda Mazembe imekamilika na klabu yake, Simba SC imeridhia.
    “Hajib si mchezaji wangu, ila Simba SC wameniomba nimsaidie kupata nafasi hiyo. Na kwa kweli kwa uwezo wake anaounyesha kwa sasa, naamini anaweza kufanikiwa,”amesema Kisongo.
    Mbali na Hajib, Kisongo amesema kwamba winga wa zamani wa Simba SC, Haroun Chanongo naye ameondoka jana pamoja na beki Abuu Ubwa kwenda Lubumbashi kufanya majaribio ya kujiunga na Mazembe.
    Wawili hao ambao kwa sasa wanachezea Stand United ya Shinyanga watakuwa Lubumbashi kwa wiki moja wakijaribiwa kabla ya majibu kutolewa.  
    Haroun Chanongo (kushoto) na Abuu Ubwa (kulia) wakiwa kwenye ndege jana wakati safari ya Lubumbashi

    Aidha, Kisongo amesema kiungo wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Mohammed Ibrahim naye yuko katika mpango wa kwenda kujaribiwa Mazembe.
    “Kwa kweli kufanya vizuri kwa Ulimwengu na Samatta kumeifanya Mazembe imekuwa na imani kubwa na wachezaji wa Tanzania,”amesema Kisongo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJIB AITWA MAZEMBE KUZIBA PENGO LA SAMATTA…CHANONGO TAYARI YUKO LUBUMBASHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top