• HABARI MPYA

    Thursday, November 05, 2015

    TAIFA STARS YAENDELEA VYEMA NA MAANDALIZI YAKE AFRIKA KUSINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinaendelea vizuri na maandalizi yake katika kambi ya Afrika Kusini kuelekea mchezo dhidi ya Algeria katikati ya mwezi huu.
    Taifa Stars itacheza mechi mbili ndani ya siku tatu na Algeria Novemba 14 Dar es Salaam na Novemba 17 Algiers kusaka nafasi ya kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
    Na nafasi hiyo inafuatia kuitoa Malawi katika hatua ya kwanza ya mchujo kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Dar es Salaam na kufungwa 1-0 Algiers.
    Mkuu wa msafara wa Taifa Stars nchini Afrika Kusini, Ahmed Iddi Mgoyi ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwamba maandalizi yanaendelea vizuri.
    Wachezaji wa Taifa Stars wakijifua mjini Johannesburg jana 
    Beki Kevin Yondan mbele akijifua kwa bidii jana Johannesburg

    “Maandalizi yanaendelea vizuri, vijana wanafanya mazoezi vizuri mara mbili kwa siku, wapo katika kambi nzuri yenye hadhi. Kwa kweli wanafurahia hapa, na sisi kama viongozi inatupa moyo,”amesema Mgoyi alipozungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwa simu kutoka Johannesburg.
    Taifa Stars imeweka kambi katika hoteli ya Holiday Inn eneo la Woodmead, Johannersburg na inafanya mazoezi kwenye viwanja jirani na maeneo hayo.
    Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa anawakosa wachezaji wawili tu kati ya 28 alioteuwa kwa maandalizi ya mchezo huo, ambao ni washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
    Wawili hao wanatarajiwa kujiunga na kambi ya timu mara baada ya mchezo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya klabu yao, TP Mazembe dhidi ya USM Alger mjini Lubumbashi mwishoni mwa wiki. Mazembe ilishinda 2-1 mchezo wa kwanza Algiers. 
    Kiungo mshambuliaji wa Free State Stars ya Afrika Kusini, Mrisho Khalfan Ngassa tayari amejiunga na kambi ya timu mjini Johannersburg tangu jana pamoja na kinara wa mabao LIgi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Elias Maguri wa Stand United aliyechelewa kuondoka na wenzake.
    Kikosi kamili cha Stars kilichopo kambini Johannersburg ni; Aishi Manula (Azam FC), Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar). 
    Mabeki ni Shomary Kapombe (Azam FC), Juma Abdul, Mwinyi Hajji Mngwali, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan (Yanga SC), Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka (Simba SC) na Salim Mbonde (Mtibwa Sugar). 
    Viungo ni Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude, Said Ndemla (Simba SC) na Salum Telela (Yanga SC). 
    Washambuliaji ni Farid Mussa, John Bocco (Azam FC), Simon Msuva, Malimi Busungu (Yanga SC), Elias Maguri (Stand United) na Ibrahim Hajib (Simba SC). 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAENDELEA VYEMA NA MAANDALIZI YAKE AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top