• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 26, 2015

  YANGA SC KUFUTA UNYONGE KWA SIMBA SC LEO?

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  ILIKUWA miezi, wiki, siku- na hatimaye sasa zimebaki saa kadhaa tu kabla ya nyasi za Uwanja bora kabisa Afrika Mashariki, Taifa, Dar es Salaam kuwaka moto kwa patashika ya pambano la watani wa jadi.
  Refa mwenye beji ya FIFA, Israel Mujuni Nkongo Saa 10:00 jioni ya leo atapuliza kipyenga cha kuanzisha mchezo wa mahasimu, Simba na Yanga Uwanja wa Taifa.
  Huo ni mchezo wa duru la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, utakaokutanisha timu zilizo kwenye kasi nzuri, baada ya zote kushinda kwa wastani mzuri tu mechi zake tatu za awali.
  Yanga SC ambayo imecheza nyumbani mechi zote, ilishinda 2-0 dhidi ya Coastal Union, 3-0 dhidi ya Prisons na 4-1 dhidi ya JKT Ruvu, wakati Simba ilishinda mechi mbili Tanga 1-0 dhidi ya African Sports na 2-0 dhidi ya Mgambo JKT, kabla ya kuichapa 3-1 Kagera Sugar Dar es Salaam.
  Ni kweli Yanga SC hata iwe bora kiasi gani haiwezi kuifunga Simba SC

  Kocha Muingereza wa Simba SC, Dylan Kerr katika mechi za mwanzo hakuwa na wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza kutokana na baadhi yao kuwa majeruhi, lakini ameweza kuiongoza timu kucheza vizuri na kushinda.
  Mchezo wa kwanza dhidi ya Sports safu yake ya ulinzi ilimkosa Nahodha Msaidizi, Hassan Isahaka, viungo Jonas Mkude, Abdi Banda na mshambuliaji Ibrahim Hajib.
  Isihaka na Hajib walipona na kucheza mchezo wa pili, wakati mchezo wa tatu aliwakosa beki mwingine tegemeo wa kati, Juuko Murushid na mshambuliaji mkongwe Mussa Hassan Mgosi.
  Wachezaji wote hao wamefanya mazoezi katika kambi ya Unguja na wako fiti kuelekea mchezo wa leo- maana yake Kerr ana wigo mpana wa wachezaji kwa ajili ya mchezo dhidi ya Yanga SC.
  Peter Manyika; Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Simon Sserunkuma, Said Ndemla, Ibrahim Hajib, Hamisi Kiiza na Mussa Hassan Mgosi hicho ndicho kikosi cha Simba SC kinachoweza kuanza leo.
  Lakini bado Kerr anaweza kuamua kutumia viungo watatu na kupunguza mshambuliaji mmoja. Tutaona muda ukifika. 
  Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amekuwa katika wakati mzuri mwanzoni mwa Ligi Kuu, kwani hana majeruhi na amekuwa akipanga vikosi vyake atakavyo katika mechi zake za awali.
  Hakuwa na mabadiliko kutoka kikosi cha ushindi wa mechi ya kwanza, ya pili hadi ya tatu na sasa mashabiki wa Yanga SC wamekwishaijua ‘first eleven’ ya mwaka huu.
  Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Godfrey Mwashiuya au Deus Kaseke. 
  Lakini leo kunaweza kukawa na mabadiliko katika safu ya ulinzi, kutokana na taarifa za Nahodha Cannavaro kuumia mazoezini kisiwani Pemba. Kuna wasiwasi pia, Niyonzima anaweza kuanzia benchi.
  Simba SC wanaamini wanaweza kufunga na timu yoyote, lakini si Yanga SC

  Haitakuwa ajabu leo, Barthez akianza pamoja na Juma Abdul kulia, Mwinyi kushoto, wakati katikati atalindwa na Twite na Yondan. Kamusoko amecheza vizuri mechi zote za awali, lakini leo anaweza kusogezwa juu, ili chini acheze Said Juma ‘Makapu’.
  Kuna uwezekano pia Yanga SC ikaanza na viungo watatu, Salum Telela akiongezeka na kupunguza idadi ya mawinga, kwa sababu Simba SC ni timu yenye mtaji mzuri wa viungo.
  Mussa Hassan Mgosi (kulia) anatarajiwa hatari zaidi kwa Yanga SC leo

  MUSSA HASSAN MGOSI:
  Wachezaji wengi wamekuwa wakitajwa wiki yote hii kuelekea pambano la watani, kwa upande wa Simba SC, Hamisi Kiiza ‘Diego’ ndiye ameonekana kama mtaji mkubwa.
  Lakini ukweli ni kwamba mtu hatari zaidi kwenye kikosi cha Simba SC kuelekea mchezo wa leo ni Mussa Hassan Mgosi, mchezaji mwenye uzoefu wa mechi za watani wa jadi kwa miaka 10 sasa.
  Kama mchezaji, Mgosi ni fundi, hodari na mzoefu ambaye anawajua vizuri mabeki wa Yanga SC. Na zaidi Mgosi wa sasa si yule wa miaka mitatu iliyopita aliyekuwa anapenda kufunga mwenyewe tu- hapana huyu wa sasa anawatengenezea zaidi nafasi wengine.
  Kiiza, Hajib na hata Awadh Juma wote, yeyote anaweza kutumbukiza mpira kwenye nyavu za Yanga SC, lakini mchezaji ambaye anatarajiwa kuwa na mvuto zaidi leo uwanjani kwa Simba SC, ni Mgosi.   
  Amissi Tambwe anatarajiwa kuwa tishio zaidi kwa Simba SC leo

  AMISI JOSELYN TAMBWE
  Mashabiki wa Yanga SC wameweka turufu zao zaidi kwa Donald Ngoma- kweli Mzimbabwe huyo ni hatari na anaweza kuwa tabu sana kwa Simba SC jioni ya leo.
  Lakini mtu hatari zaidi kwa Simba SC leo ni Mrundi Amissi Joselyn Tambwe, ambaye hapana shaka kocha Hans van der Pluijm atamuanzisha kwa sababu anajua umuhimu wake awapo uwanjani.
  Tambwe wa msimu huu, amekuwa anacheza kwa kuwafikiria kwanza wenzake kufunga na ndiye anaongoza hadi sasa kutoa pasi za mabao, lakini pia naye anafunga.
  Tambwe amekutana na misukosuko mingi ya mabeki wa Tanzania na anawajua vizuri- isitoshe hao wa Simba SC amecheza nao anawajua kivitendo na maneno. Hakuna mtu wa kumtisha katika safu ya ulinzi ya Simba SC.
  Uchezaji wa Tambwe umebadilika kwa kiasi kikubwa kutoka alivyokuwa Simba SC, na akiwa katika msimu wake wa pili Jangwani, tayari Mrundi huyo anajisikia yuko nyumbani.
  Kocha wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr akiwa mbele ya benchi lake

  BAO LA MAPEMA NDIYO SILAHA;
  Kutokana na ukweli kwamba Simba na Yanga leo zinakutana zikiwa zipo vizuri na ikumbukwe hii ni Ligi Kuu, hapa ni vita ya pointi, atakayejiruhusu kufungwa mapema, atateseka.
  Unatarajiwa kuwa mchezo wa nidhamu ya hali ya juu katika kushambulia na kujihami, ila atakayekubali kupokea bao la mapema, atateseka, maana kitakachofuata ni mpinzani kulinda pointi tatu.
  Na baada ya timu hizo kukabana koo katika mizunguko mitatu tangu kuanza kwa Ligi Kuu, leo ni nafasi ya kuanza kujua timu ipi inaongoza kwenye msimamo na ipi inafuatia.  
  Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm (kushoto) akiwa na benchi lake zima la Ufundi

  YANGA NI WANYONGE KWA SIMBA
  Tayari kuna imani, Yanga SC inaweza kushinda mechi yoyote ngumu, lakini si kwa Simba SC na hiyo ndiyo picha halisi kuelekea mchezo wa leo. Mashabiki wa Yanga hawana amani na timu yao kwa asilimia 100 mbele ya Simba SC.
  Na Simba SC wanajiamini, wanaweza kufungwa na timu hata ya Daraja la Nne, lakini siyo Yanga SC. Simba SC wanaamini wanaweza kuifunga Yanga SC wakiwa na wachezaji wa aina yoyote.
  Na kwa kiasi kikubwa hapo ndipo ulipolalia utamu wa mechi ya leo, kwamba baada ya uwekezaji wote katika usajili wa Yanga SC wataendelea kuwa wanyonge kwa Simba SC?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC KUFUTA UNYONGE KWA SIMBA SC LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top