• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 28, 2015

  BEKI BUTU ILIIPONZA SIMBA SC KUPIGWA 2-0 NA YANGA JUMAMOSI, ASEMA MEXIME

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Mecky Mexime Kianga amesema kwamba safu mbovu ya ulinzi iliwaponza Simba SC kufungwa mahasimu wao, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba ilifungwa 2-0 na Yanga SC katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mabao ya Amissi Tambwe kipindi cha kwanza na Malimi Busungu kipindi cha pili.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwa simu kutoka Turiani, Morogoro, Mexime amesema kwamba Simba SC wanatakiwa kufanyia kazi safu yao ya ulinzi, vinginevyo itaendelea kuwagharimu. "Kilichowaumiza Simba ni kutokuwa na safu imara ya ulinzi," amesema.
  Kikosi cha Simba SC kilichofungwa 2-0 na Yanga SC Jumamosi

  Kuelekea mchezo wake na Yanga SC, Mexime amesema kwamba Mtibwa Sugar ina ukuta imara hivyo haitapa shida kwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu.
  "Mabeki wangu wako vizuri zaidi ukilinganisha na waliocheza juzi kwa upande wa Simba, yaani (alitaja jina la beki) ndio wanamtegemea, kwangu bado hajanivutia," aliongeza beki huyo na nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
  Mtibwa Sugar wanatarajia kuikaribisha Yanga keshokutwa Jumatano katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
  Amesema ameiona Yanga katika mechi ilizocheza hivyo anajua mbinu za kuwakabili na hatimaye kuibuka na ushindi, kwani anawaamini wachezaji wake ambao wamejipanga kusaka ushindi na vile vile kutangaza vipaji vyao.
  Mecky Mexime, kocha wa Mtibwa

  "Naijua Yanga, wapi iko imara na wapi wana udhaifu, njooni Morogoro Jumatano muone vijana wanavyojua kutawala mpira, wadogo na wa mtaani lakini mambo yao uwanjani ni makubwa," amesema Mexime.
  Mtibwa Sugar, kama Yanga SC zote zimeshinda mechi zao zote nne za mwanzo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayorushwa moja kwa moja na Azam TV, sawa na Azam FC na Jumtano zinatarajiwa kukutana mchezo wa kuwania usukani wa ligi hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BEKI BUTU ILIIPONZA SIMBA SC KUPIGWA 2-0 NA YANGA JUMAMOSI, ASEMA MEXIME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top