• HABARI MPYA

  Jumanne, Septemba 29, 2015

  HANS POPPE AWATAKA MBEYA CITY ‘WAJIVUE GAMBA’ KWA JUMA NYOSSO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amewataka Mbeya City FC kumchukulia hatua beki wao, Juma Said Nyosso kabla ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Nyosso alimtomasa nyuma Bocco katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juzi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Azam FC ikillaza 2-1 Mbeya City.
  Na Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo kwamba pamoja na wadau wengi kuishinikiza TFF imchukulie mchezaji huyo, lakini klabu yake inapaswa kuchukua hatua kwanza.
  Hans Poppe amewataka Mbeya City wamchukulie hatua Juma Nyosso 

  Poppe amesema Simba SC iliamua kumuacha Nyosso akiwa mchezaji mzuri, lakini tu kwa tabia zake hizo za ajabu.
  “Tulikuwa tunazungumza naye sana, aache. Hasikii. Tukaona huyu ni mtu ni tatizo sugu tukaachana naye, sasa hao waliomsajili wameshuhudia kwao akiendelea na mambo hayo bila kuchukua hatua,”.
  “Haya matukio mawili ni ambayo yamenaswa na kamera akiwa Mbeya City, lakini unadhani ni wachezaji wangapi amewafanyia hivi bila kunaswa na kamera?”alihoji Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
  Poppe amesema Mbeya City lazima iuonyeshe kwanza umma wa wapenda soka Tanzania kwamba wao wamekerwa zaidi na matukio hayo na si kusubiri aadhibiwe na TFF, amalize adhabu waendelee kuwa naye.
  “Hatutakiwi kabisa kuyaachia mambo ya kihuni katika soka. Huu sasa ni mchezo wa kisayansi, ajira na biashara kubwa dunia nzima. Unapaswa kuheshimiwa. Matukio ya Nyosso yanaitia doa sana kwanza Mbeya City yenyewe, inaonekana pia ni timu ya kihuni,”.
  “Lazima Mbeya City ionyeshe imekerwa kwa kumchukulia hatua Nyosso, vinginevyo haitasaidia hata akiadhibiwa na TFF. Sisi tulikubali kumpoteza mchezaji mzuri kama yeye, tu kwa sababu ya kuipa heshima yake soka,”amesema Poppe. Mdau mwingine wa soka, Charles Hamkah amesema tukio alilofanya Juma Nyosso si la kuvumiliwa tena na hapaswi kuacha aendelee kucheza soka Tanzania. "Huyu mtu wa kufungia maisha kabisa, kwa sababu amekwishaonywa sana, anarudia, sasa wamfungie maisha,"amesema Mkurugenzi wa huyo wa kampuni ya Utalii ya CXC Africa.
  Charles Hamkah anataka Juma Nyosso afungiwe maisha kwa sababu amekwishaonywa sana na anarudia
   

  Tukio la Jumapili ni la nne kuonekana Nyosso akiwafanyia wachezaji wenzake, kwanza mwaka 2007 akiwa Ashanti United alimfanyia Joseph Kaniki akiwa Simba SC, mwaka 2010 akiwa Simba SC alimfanyia Amir Maftah akiwa Yanga Sc na msimu uliopita akiwa hapo hapo Mbeya City, alimfayia Elias Maguri akiwa Simba SC.
  Mbeya City haijatoa tamko lolote hadi sasa, lakini Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema beki huyo ngangari atachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HANS POPPE AWATAKA MBEYA CITY ‘WAJIVUE GAMBA’ KWA JUMA NYOSSO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top