• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 27, 2015

  SIMBA SC WASITAFUTE MCHAWI, WAHESHIMU MATOKEO YA UWANJANI

  SIMBA SC imepoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, baada ya kufungwa mabao 2-0 na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba SC sasa inazidiwa kwa pointi tatu na Yanga SC na Mtibwa Sugar, huku ikiwa inalingana na Azam FC, ambayo nayo inaweza kuwaacha Wekundu hao wa Msimbazi, iwapo itashinda dhidi ya Mbeya City leo.
  Mashabiki wa Simba SC hawana raha kwa mwaka wa tatu sasa, kutokana na timu yao kutofanya vizuri katika Ligi Kuu na wanatamani mabadiliko msimu huu.

  Bahati nzuri, tofauti na msimu uliopita ilipoanza kwa sare sita mfululizo, msimu huu Simba SC imeshinda mechi zote tatu mwanzoni, zikiwemo mbili za ugenini.
  Ilishinda 1-0 dhidi ya African Sports na 2-0 dhidi ya Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kabla ya kushinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar Dar es Salaam.
  Na katika mchezo wa jana, pamoja na kufungwa, Simba SC walicheza vizuri kuliko mahasimu wao, lakini unaweza kusema tu makosa kidogo ya umakini katika safu ya ulinzi yaliwaangusha.
  Lakini pia hata umakini mdogo wa wachezaji wa mbele katika kutumia nafasi, au uhodari wa kipa wa Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ viliwaangusha.
  Simba SC walikosa mabao matatu ya wazi, mawili kipindi cha kwanza na moja kipindi cha pili.
  Na mabeki wake hawakuwadhibiti vyema wafungaji wa mabao ya Yanga SC jana, Amisi Tambwe na Malimi Busungu wakati wanafunga.
  Mpira wa miguu ni mchezo wa makosa na ndiyo maana kuna walimu ambao kazi yao ni pamoja na kurekebisha makosa kila baada ya mchezo mmoja kuelekea mchezo mwingine.
  Kwa kawaida, Simba na Yanga huwa hazipendi kufungwa na inapotokea hivyo, basi hutafutwa sababu na mwisho wa siku wachezaji ‘hutolewa kafara’.
  Mara baada ya mchezo, baadhi ya mashabiki wa Simba SC walianza kuwanyooshea vidole baadhi ya wachezaji eti walicheza chini ya kiwango.
  Na mara nyingi baada ya tetesi na tuhuma, kinachofuatia ni uongozi kufukuza au kusimamisha wachezaji.
  Niwapongeze Yanga SC ni kama wameamua kuondoka na desturi hiyo. Sasa wanayakubali matokeo ya uwanjani, na licha ya kufungwa na mahasimu wao, mfululizo siku karibuni, lakini hawajatoa kafara wachezaji ingawa makocha wawili walifukuzwa baada ya kufungwa na Simba SC, ambao ni Mholanzi Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts na Mbrazil Marcio Maximo Barcellos.
  Pamoja na kuipa Yanga SC ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2012-2013, lakini Brandts alitupiwa virago baada ya kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba SC Desemba 23 katika mchezo wa Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Mabao ya Simba SC siku hiyo yalifungwa na Amisi Tambwe mawili dakika ya 14 na 44 kwa penalti na Awadh Juma, wakati bao pekee la Yanga lilifungwa Emmanuel Okwi dakika ya 87.
  Maximo alifukuzwa kufuatia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba SC Desemba 13, mwaka jana katika mchezo wa Nani Mtani Jembe 2, mabao ya Awadh Juma na Elias Maguri.  
  Lakini Simba SC ni mwaka jana tu wamewafukuza Amri Kiemba na Haroun Chanongo kwa madai ya kucheza chini ya kiwango kuhujumu timu.
  Kwa walioitazama vizuri mechi ya jana, watakubaliana nami kwamba Simba SC ilifungwa kimchezo na kinachopaswa kufuata sasa ni kocha Muinereza, Dylan Kerr kufanyia mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo jana.
  Lakini iwapo viongozi wa Simba SC watathubutu kuukataa uhalisia wa mchezo na kutaka kuwatoa kafara wachezaji wake, watajivuruga mno na kujitoa kwenye mbio za ubingwa.
  Katika mechi dhidi ya mahasimu wao hao, Yanga imekuwa kawaida viongozi wa Simba SC kuwaahidi zawadi na donge nono la fedha wachezaji wake.
  Maana yake wachezaji wa Simba SC waliondoka uwanjani na vilio vya aina mbili, kwanza kupotea mechi na pili kukosa donge nono la fedha taslimu.
  Lakini ni wachezaji hao hao ambao Simba SC inawategemea kwa kampeni nzima ya Ligi Kuu msimu huu.
  Hii inamaanisha kwamba, viongozi wa Simba SC hawapaswi kabisa kuwavuruga wachezaji wao, badala yake waelekeza nguvu zao katika mchezo ujao dhidi ya Stand United Jumatano.
  Na si hivyo, tu mchezo wa mahasimu ni mchezo maalum ndiyo maana hata maandalizi yake huwa yanakuwa maalum.
  Na wachezaji wanaposhindwa hupata donge nono. Wanapopoteza mechi ni nadra kupewa fedha. Wachezaji wa Simba SC waliingia katika mchezo wa jana kwa matumaini makubwa ya ushindi maana yake walikuwa wana matumaini pia ya kupata posho nzuri.
  Ili kuwarudisha haraka mchezoni, viongozi wa Simba SC watumie busara tu kwa kufikiria kuwapa chochote wachezaji wake licha ya kupoteza mchezo.
  Kikubwa ninachotaka kuwaambia viongozi wa Simba SC leo, pamoja na kuwapa pole ni kwamba, waheshimu matokeo ya uwanjani na wasiwavuruge wachezaji wao, watajivuruga zaidi. Alamsiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WASITAFUTE MCHAWI, WAHESHIMU MATOKEO YA UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top