• HABARI MPYA

    Monday, September 21, 2015

    CHRISTIAN BELLA PIGA PESA, USIKUBALI WANAOKUCHUKIA WAKUTOE KWENYE RELI

    IPO tabia moja ambayo sijui dawa yake itapatikana lini – tabia ya kuwachukia wenye kujua, kuwaonea choyo, kuwaombea mabaya, yaani mtu anakonda  kwa mafanikio ya mwenzie, ananenepa kwa anguko la mwenzie.
    Kwenye sanaa tabia hii ndio imevuka mipaka, kuna chuki za kufa mtu na leo hii napenda kumtaja mwimbaji Christian Bella kama mmoja wa watu wanaokumbana na kadhia ya tabia hiyo ya kikorosho. 
    Bella anaambiwa ana roho mbaya, anaringa lakini mbaya zaidi ni kwamba baadhi ya wasanii wa dansi na baadhi ya mashabiki wa muziki wa dansi wanatamani kumtenga Bella – eti hapigi dansi, anapiga bongo fleva - mada ya kijinga kabisa ambayo kama utaifuatilia kwa kina hutapata jibu la uhakika kuwa muziki wa dansi ni upi na bongo fleva ni ipi.
    Niliwahi kuandika huko nyuma kuwa Malaika Music Band imefanikwa kufika hapo ilipo kwa sababu ya CHRISTIAN BELLA – mwimbaji mwenye sauti nzuri, mwenye tungo nyingi nzuri, mwenye nyota kali na mwenye kujua nini kinahitajika sokoni.
    Nikaandika pia kuwa hadi miezi kadhaa nyuma Malaika Band ilikuwa ina nyimbo mbili tu zilizoko radioni “Nakuhitaji” na “Mtu wa Watu”, lakini pia bendi hiyo ilikuwa na wimbo mmoja tu kwenye video “Nakuhitaji”.
    Unaweza kujiuliza ni vipi Malaika ishike soko kwa kiasi kikubwa huku ikiwa na nyimbo mbili radioni na moja videoni, ni jambo linalowezekana lakini hapa jibu ni jepesi – Malaika Band ilibebwa na hazina ya nyimbo nyingi nzuri za Bella kuanzia Akudo Impact hadi kwenye nyimbo zake binafsi nje ya bendi.
    Na ndio maana unapoingia kwenye show za Malaika, nyimbo zinazochengua watu mbali na  “Nakuhitija” na “Mtu wa Watu” zimo pia “Nashindwa”, “Yako Wapi Mapenzi”, “Usilie”, “Msaliti” “Nani Kama Mama” na nyingine nyingi, zote hizo ni kazi ya Christian Bella.
    Anachokifanya Bella ni kusoma soko la muziki linahitaji nini kisha anapenya hapo hapo na iwapo wasanii wa dansi wataendelea kukaa kitako na kumtenga basi wataishia kusema jamaa hapigi dansi huku mwenzao akitengeneza pesa.
    Enzi za kufanya muziki kama wito zimepita, muziki wa sasa ni ajira, muziki ni maisha, ubunifu wa hali ya juu unahitajika na msanii anapaswa kubadilika kadri soko linavyobadilika.
    Hivi karibuni Bella kupitia Malaika Band ameachia wimbo “Amerudi” ambao umekuwa ni ‘shidah’ mjini, kila mtu anaimba Amerudi, Malaika inazidi kupaa, Bella anazidi kutimua vumbi.
    Jumapili nikiwa nyumbani nikitazama Top 20 ya Clouds TV ambayo husheheni nyimbo kali za bongo fleva, nikapigwa na butwaa pale nilipoona “Amerudi” ya Malaika Band imeshika nafasi ya 16.
    Hakika sijawahi kuona wimbo wa bendi za dansi kwenye hiyo chati ya Clouds TV, nathubutu kusema haijawahi kutokea.
    Kitendo cha ngoma hiyo kupenya kwenye chati zinazotawaliwa na muziki wa bongo fleva, kunaonyesha kuwa kama wasanii wa dansi watatoa nyimbo kali basi ule usemi kuwa dansi linabadiniwa, utafutiliwa mbali.
    Lakini Bella huyo huyo nikamuona tena na wimbo wake “Nashindwa” akiwa ameshika namba mbili kwenye chati hizo hizo za Top 20 ya Clouds TV …Hii maanake nini? Maanake ni kwamba Bella anajua, na tunasatahili tumpe heshima yake.
    Bella ushauri wangu wa bure kwako ni huu: piga pesa, usikubali wasiokupenda wasikutoe kwenye reli, akija mwenye wivu wa maendelea mbebe, akija mwenye wivu wa kishetani mpotezee.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHRISTIAN BELLA PIGA PESA, USIKUBALI WANAOKUCHUKIA WAKUTOE KWENYE RELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top