• HABARI MPYA

  Jumanne, Septemba 29, 2015

  HII NDIYO HUKUMU YA MCHUNGAJI NTEZE JOHN LUNGU KWA JUMA SAID NYOSSO, ASEMA…

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba SC, Mchungaji Nteze John Lungu amelaani vikali kitendo cha beki wa Mbeya City, Juma Said Nyosso kumdhalilisha mshambuliaji wa Azam FC, John Raphael Bocco.
  Nyosso alimtomasa nyuma Bocco katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara juzi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Azam FC ikillaza 2-1 Mbeya City.
  Na akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwa simu kutoka Bellevue, Washington, Marekani, Nteze aliyewahi pia kuchezea Pamba ya Mwanza amesema kwamba Nyosso anastahili adhabu kali.
  Mchungaji Nteze John (kushoto) amesema Juma Nyosso anastahili adhabu kali ili iwe fundisho 

  “Inabidi TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) imchukulie hatua kali, anastahili kufungiwa ili iwe fundisho wachezaji wahuni,”amesema Nteze.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa Free State Stars ya Afrika Kusini enzi ikiitwa Qwa Qwa Stars, amesema kwamba mpira wa miguu unafundisha watoto wetu tabia njema na sio kama ya Nyosso.
  “TFF kwanza inabidi iwe inafuatilia kwa karibu matukio ya aina hii, na lazima ichukue hatua kali ambazo zitawafanya wengine waogope, tukiachia haya yaendelee, tutakuwa tunapandikiza mizizi mibaya katika soka yetu,”amesema Nteze ambaye tayari ni raia wa Marekani.
  “Soka ni mchezo ambao unatakiwa uwe wa kistarabu, watu tushindane kwa ujuzi na siyo uhuni na uchafu kama huo wa Nyosso. Inabidi afungiwe ili iwe fundisho kwa wahuni wenzake,”ameongeza Nteze. 
  Nteze John Lungu kwa sasa ni Mchungaji nchini Marekani

  Wachezaji wengine wengi tu wamelaani kitendo cha Nyosso na ingawa inafahamika awali aliwahi kuwafanyia hivyo Joseph Kaniki mwaka 2007 na Elias Maguri msimu uliopita wote wa Simba, lakini jana beki wa zamani wa Yanga SC, Amir Maftah naye ameibuka na kumshutumu Nyosso kuwahi kumfanyia hivyo. 
  Kipa wa zamani Yanga na Simba, Ivo Mapunda, kiungo wa zamani wa Pamba SC, Mao Mkami na kinda wa Mwadui FC ya Shinyanga Hassan Kabunda nao wamelaani vikali kitendo cha Nyosso.
  Nteze John wa pili kushoto katika mwaka wake wa mwisho kuichezea Simba SC, 2004
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HII NDIYO HUKUMU YA MCHUNGAJI NTEZE JOHN LUNGU KWA JUMA SAID NYOSSO, ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top