• HABARI MPYA

    Tuesday, September 22, 2015

    …LUNYAMILA: UZURI WA YANGA SC HAITEGEMEI MTU MMOJA

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    WINGA wa zamani wa Yanga SC, Edibily Jonas Lunyamila amesema kwamba uzuri wa ‘fowadi’ ya timu yake kwa sasa haitegemei mtu mmoja kama mahasimu wao, Simba SC ambao wanamtegemea Hamisi Kiiza ‘Diego’ pekee.
    Akizungumzia mchezo wa mahasimu hao wa jadi utakaofanyika mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, Lunyamila amesema kwamba Yanga SC ina washambuliaji watatu, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Simon Msuva ambao wote wanafunga.
    “Sisi hatutegemei mtu mmoja kama wenzetu wana Kiiza tu, sisi tuna Tambwe, Msuva na Ngoma wote wanafunga, kwa hiyo tuna matumaini ya ushindi Jumamosi,”amesema.
    Pamoja na hayo, Lunyamila ametoa tahadhari kwa viongozi na wanachama walio karibu na timu kuacha kuwavuruga wachezaji kuelekea mchezo huo.
    Edibily Lunyamila amesema Yanga SC haitegemeo mfungaji mmoja kuelekea mechi na Simba
    Edibily Lunyamila (kushoto) akiwa na Mohammed Hussein 'Mmachinga' enzi zao wanacheza Yanga SC mwaka 1993



    “Kuelekea mechi hizi huwa kunakuwa na maneno maneno mengi sana, wachezaji wanaambiwa wamechukua hela na nini, hiyo huwa inachangia sana kuwavuruga wachezaji. Naomba safari hii Yanga wasiruhusu kitu kama hicho, wawaache wachezaji wawe huru wakati huu,”amesema Lunyamila.    
    Yanga SC inatarajiwa kumenyana na mahasimu wao wa jadi, Simba SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Yanga SC itaingia katika mchezo huo ikitoka kushinda mechi zake zote tatu za awali, 2-0 dhidi ya Coastal Union, 3-1 dhidi ya Prisons na 4-1 dhidi ya JKT Ruvu.
    Kwa sasa kikosi cha Yanga SC kimeweka kambi kisiwani Pemba tangu Jumapili kwa maandalizi ya mchezo huo ambao utaonyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam TV, wakati mahasimu wao nao, Simba SC wapo Unguja.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: …LUNYAMILA: UZURI WA YANGA SC HAITEGEMEI MTU MMOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top