• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 28, 2015

  WASANII CHUNGENI NDIMI ZENU KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI MKUU

  MAJUZI nilitumiwa video fupi ya katuni kupitia Whatsapp ikionyesha watu kadhaa wakiwa kwenye safari fulani huku wamebeba misalaba mirefu mabegani mwao.
  Ni wazi kuwa misabala ile iliwapa uchovu kiasi kilichopelekea mvivu mmoja kuupunguza msabala wake kwa msumeno kila baada ya hatua kadhaa.
  Akaendelea kufanya vile tena na tena hadi msalaba ule ukawa mfupi, akapata wepesi wa kuchapa mwendo na kuwaona wenzake majuha.
  Muda mfupi baadae wakafika kwenye daraja refu, wenzake wakalaza ile misalaba yao na kuifanya kama kivuko na walipofika ng’ambo ya pili wakaivuta misalaba na kuendelea na safari huku yule mjanja wa kupunguza msalaba safari yake ikikomea hapo.

  Nailinganisha video ile na maisha ya wasanii katika kipindi hiki kifupi cha kabla na baada uchaguzi mkuu wa taifa.
  Tuna chini ya siku 30 kabla uchaguzi mkuu haujafanyika hapo Oktoba 25, joto la uchaguzi linazidi kupanda, watu wameshikwa na mhemko kupindukia.
  Kwa mara nyingine tena tunashuhudia namna wasanii wa fani mbali mbali wanavyodhihirisha umuhimu wao katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
  Kwa njia moja au nyingine, wasanii wamekuwa wakihusika katika kampeni ya kila chama, kila mgombea, kila ngazi.
  Kuna manufaa yoyote wanayopata wasanii kwa kushiriki kampeni hizi? Naam yapo, tena makubwa tu, hiki ni kipindi cha mavuno, wasanii wanatengeneza pesa za kutakata.
  Hakuna kosa kwa wasanii kushiriki kampeni, wala sioni tatizo msanii kuonyesha utashi wake juu ya mgombea fulani, lakini tahadhari ya hali ya juu inahitajika katika hili.
  Kampeni za mwaka huu zimetaliwa na matusi na vijembe vya kila aina kuliko kipindi chochote kile, msanii yoyote yule anayejidumbukiza kwenye matumizi ya lugha za matusi, vijembe na maneno ya kifedhuli basi atakuwa hana tofauti na yule bwana aliyekuwa anaupunguza msalaba wake kwa msumeno.
  Wasanii wanapaswa kujua kuwa wana mashabiki kutoka pande zote, kwa kila chama, kwa kila mgombea na hivyo wanastahili kuhakikisha hawapotezi mashabiki wao kwa kujiingiza katika kampeni chafu.
  Wako wasanii wanaoona msimu wa kampeni ndiyo msimu wa kutoka kimaisha na hivyo wako tayari kujilipua kwa aina yoyote ile ili mradi waendelee kupata dili za kushiriki kampeni. 
  Ni vema aina hii ya wasanii wakajua kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na kwamba baada ya hapo watalazimika kurejea tena kwa wateja wao ambao ni wapiga kura.
  Kumtusi mgombea au chama ni sawa na kumtusi mfuasi wa mgombea au mfuasi wa chama, kitakachofuata baada ya hapo ni chuki itakayodumu milele na milele - wahenga walisema usimuudhi mchinja mbwa wazimu utakurudia, wasanii kuweni makini na ndimi zenu vinginevyo mtakomea darajani na misalaba yenu mifupi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WASANII CHUNGENI NDIMI ZENU KUNA MAISHA BAADA YA UCHAGUZI MKUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top