• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 25, 2015

  SIMBA NA YANGA ZAREJEA TAYARI KWA KIPUTE CHA KESHO TAIFA

  Na Waandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WATANI wa jadi, Simba na Yanga SC wote wanarejea leo Dar es Salaam kutoka kwenye kambi zao Zanzibar kuelekea pambano lao la kesho.
  Miamba hiyo inatarajiwa kumenyana kesho jioni Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanzia Saa 10:00.
  Yanga SC ilikuwa imeweka kambi kisiwani Pemba wakati mahasimu wao, Simba SC walikuwa Unguja kwa wiki yote hii kujiandaa na mchezo huo.
  Hakuna majeruhi wa kutisha katika kambi zote mbili na makocha wote, Muingereza Dylan Kerr wa Simba SC na Hans van der Pluijm wa Yanga SC wamefurahia maandalizi yao.
  Simba SC watapiga ndiki kama hii kesho Uwanja wa Taifa kabla ya kumenyana mahasimu wao, Yanga SC

  Mchezo huo unatarajiwa kuchezeshwa na refa mwenye beji ya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA), Israel Mujuni Nkongo wa Dar es salaam, atakayesaidiwa na Josephat Bulali wa Tanga, Ferdinand Chacha wa Mwanza, wakati mezani atakuwapo Soud Lila pia wa Dar es Salaam na Kamisaa atakuwa Charles Mchau kutoka Kilimanjaro.
  Viingilio katika mchezo huo vinatarajiwa kuwa Sh 7,000 kwa kwa viti vya rangi ya bluu, kijani na chungwa, Sh. 30,000 kwa VIP A na Sh. 20,000 kwa VIP B na C, wakati tiketi zimeanza kuuzwa tangu asubuhi ya leo katika vituo vya Ofisi za TFF Uwanja wa Karume, Buguruni – Oilcom, Dar Live – Mbagala, Uwanja wa Taifa, Luther House – Posta, Feri – Kivukoni, Mnazi Mmoja, Ubungo – Oilcom na Makumbusho – Standi ya mabasi ya daladala.
  Watani hao wa jadi, wanakutana kesho baada ya wote kuwa mwanzo mzuri katika Ligi Kuu, wakishinda medhi zao zote tatu za awali, Yanga ikizifunga 2-0 Coastal Union, 3-1 Prisons na 4-1 JKT Ruvu, wakati Simba ilizifunga 1-0 African Sports, 2-0 Mgambo JKT na 3-1 Kagera Sugar.
  Mashabiki wa Yanga SC wanatarajiwa kumiminika kwa wingi kesho Uwanja wa Taifa kuisapoti timu yao 

  Mechi nyingine za Ligi Kuu ya Vodacom kesho zitakuwa ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mwadui FC katika Uwanja wa Mkwakwani mijini Tanga, Prisons na Mgambo JKT Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, JKT Ruvu na Stand United Uwanja wa Karume, Dar es salaam, Mtibwa Sugar na Majimjaji ya Songea Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Kagera Sugar na Toto Africans Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
  Ligi hiyo itaendelea keshokutwa kwa michezo miwili, kati ya Azam FC na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na African Sports na Ndanda FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ZAREJEA TAYARI KWA KIPUTE CHA KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top