• HABARI MPYA

  Jumanne, Septemba 29, 2015

  BUSUNGU: KUIFUNGA SIMBA SC ‘SIYO ISHU’, UBINGWA NDIYO MPANZO MZIMA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Malimi Busungu amesema kwamba kuifunga Simba SC hakuwezi kumfanya ajione amemaliza, kwani ana ndoto za kufika mbali zaidi kisoka.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE mwishoni mwa wiki, Busungu amesema kwamba yeye bado mchezaji mchanga anayehitaji mafanikio zaidi.
  “Kweli nimefurahi kufunga na kuisaidia timu yangu kushinda mechi. Hilo ndilo kubwa, hii ni Ligi na Yanga kama timu tunahitaji kuendelea kushinda ili kutetea ubingwa,”amesema.
  Hata hivyo, Busungu amesema anahitaji kuendelea kufanya vizuri kuanzia mazoezini ili kuwashawishi makocha Yanga SC kuendelea kumpa nafasi.
  Malimi Busungu amesema hawezi kujiona amemaliza kwa kuifunga Simba SC

  “Kama unavyoona kwa Yanga SC pekee, bado sijawa mchezaji wa kikosi cha kwanza, ili furaha yangu itimie lazima kwanza niwe na uhakika wa namba katika timu. Pili nipate nafasi na timu ya taifa, baada ya hapo nifikirie kupata nafasi ya kwenda kucheza Ulaya,”amesema.
  Busungu alimsetia Amissi Tambwe kufunga bao la kwanza kipindi cha kwanza kabla ya yeye mwenyewe kumalizia kwa kichwa mpira uliorushwa na Mbuyu Twite kuipatia Yanga SC bao la pili katika ushindi wa 2-0 Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Na kesho, Yanga SC inatarajiwa kucheza ugenini kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu msimu huu, itakapomenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BUSUNGU: KUIFUNGA SIMBA SC ‘SIYO ISHU’, UBINGWA NDIYO MPANZO MZIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top