• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 24, 2015

  AZAM FC YAZIKATA MAINI SIMBA NA YANGA, DOGO FARID ATIWA PINGU NZITO CHAMAZI

  Na Prince Akbar,  DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji chipukizi wa Azam FC, Farid Malik Mussa (pichani kushoto) amesaini Mkataba mpya kuendelea kuichezea klabu hiyo kwa miaka mitatu zaidi.
  BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE inafahamu Farid amesaini Mkataba huo wiki iliyopita kabla ya timu kwenda Shinyanga kwenye mechi zake mbili za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kocha Muingereza, Stewart Hall alihakikisha kinda huyo anapewa Mkataba mpya mapema ili akili yake itulie aweze kucheza soka vizuri.
  Tayari Farid aliyeng’ara kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame alikuwa amekwishaanza kufuatiliwa na vigogo Simba na Yanga.
  Na Azam FC kuepuka kumpoteza mchezaji huyo ambaye tayari ana namba kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars imeamua kumpa Mkataba mnono.
  Habari zinasema Farid amepata Mkataba mnono kuanzia kwenye dau la kusaini, mshahara na marupurupu mengine pia. “Baada ya kupata fedha zake, dogo akaenda kununua nyumba,”kimesema chanzo.
  Farid Mussa Malik (kulia) akiruka na mpira wake kumpita beki wake wa Gor Mahia wakati wa Kombe la Kagame Agosti

  Farid ni mchezaji aliyeibuliwa kutoka akademi ya Azam FC na alianza taratibu kukomazwa kikosi cha kwanza mwaka juzi, chini ya kocha Hall. Hata hivyo, baada ya Hall kuondolewa Azam FC, Farid alipotea hadi hapo Muingereza huyo aliporejeshwa katikati ya mwaka, naye akafufua makali na sasa ni gumzo nchi nzima.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAZIKATA MAINI SIMBA NA YANGA, DOGO FARID ATIWA PINGU NZITO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top