• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 27, 2015

  MCHEZAJI COASTAL AFARIKI UWANJANI TIMU IKITOA SARE NA MWADUI, JKT YADUNDWA TENA, MTIBWA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI

  MATOKEO YA MECHI ZA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA
  Jumamosi Septemba 26, 2015
  Simba SC 0-2 Yanga SC
  Coastal Union 0-0 Mwadui FC
  Prisons FC 1-0 Mgambo JKT
  JKT Ruvu 0-1 Stand United
  Mtibwa Sugar 1-0 Majimaji FC
  Kagera Sugar 0-0 Toto Africans
  Jumapili Septemba 27, 2015
  African Sports Vs Ndanda FC
  Pumzika kwa amani Mshauri Salim
  MCHEZAJI chipukizi wa timu ya vijana ya Coastal Union ya Tanga, Mshauri Salim amefariki dunia jioni ya Jumamosi baada ya kuanguka Uwanja wa Mkwakwani kufuatia kugongana na mchezaji na mwenzake.
  Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Coastal Union dhidi ya Eagles Academy uliotangulia kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Coastal na Mwadui FC ya Shinyanga uliomalizika kwa sare ya 0-0.
  Ofisa Habari wa Coastal Union, Oscar Assenga amesema kwamba mchezaji huyo aligongana mwenzake kabla ya kuanguka na kupoteza fahamu na umauti ulimfika akiwa njiani anakimbizwa kituo cha afya cha Ngamiani.
  Taratibu za mazishi zinafanywa na Coastal Union inatarajiwa kutoa taarifa zaidi leo.
  Katika mechi nyingine za Ligi Kuu Jumamosi, Yanga SC imeilaza Simba 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mabao ya Amisi Tambwe na Malimi Busungu, wakati Mtibwa Sugar imeshinda 1-0 dhidi ya Majimaji, bao pekee la Shiza Kichuya kwa penalti dakika ya 70.
  JKT Ruvu imeendelea kuvurunda, baada ya leo kufungwa mechi ya nne mfululizo kufuatia kuchapwa 1-0 na Stand United Uwanja wa Karume, Dar es Salaam bao pekee la Elias Maguli dakika ya tisa.
  Prisons imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Mgambo Uwanja wa Sokoine, Mbeya bao pekee la Said Mkopi dakika ya 67, wakati Kagera Sugar imelazimishwa sare ya 0-0 na Toto Africans Uwanja wa Mwinyi, Tabora.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi mbili, kati ya African Sports na Ndanda FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Azam FC na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MCHEZAJI COASTAL AFARIKI UWANJANI TIMU IKITOA SARE NA MWADUI, JKT YADUNDWA TENA, MTIBWA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top