• HABARI MPYA

  Jumapili, Septemba 20, 2015

  SALAMU ZAO JANGWANI…KIIZA APIGA HAT-TRICK SIMBA YAITANDIKA KAGERA SUGAR 3-1 TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MESEJI sent. Naam, ndivyo unavyoweza kusema- baada ya Simba SC kushinda mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwa ni wiki moja kabla ya kumenyana na watani, Yanga SC.
  Akiwa katika ubora wake, mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Friday Kiiza maarufu Diego amefunga mabao yote ya Simba SC jioni ya leo na kufikisha mabao matano ndani ya mechi tatu za Ligi Kuu.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, hadi mapumzoko Simba SC walikuwa tayari wanaongoza kwa bao 1-0 lililopatikana mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
  Wachezaji wa Simba SC wakishangilia bao la tatu

  Kiiza alifunga bao hilo akimalizia kwa kichwa krosi maridadi ya kiungo Awadh Juma Issa aliyecheza vizuri mno leo.
  Pamoja na Simba SC kutoka inaongoza, dakika 45 za kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu na sifa zimuendee kipa Peter Manyika kwa kuokoa michomo kadhaa ya Kagera Sugar.
  Mtoto huyo wa kipa wa zamani wa Yanga SC, Manyika Peter aliokoa shuti la Iddi Kurachi dakika ya tano, lakini kali zaidi ni dakika ya 29 alipochupia shuti la Paul Ngway lililomtoka na kugeuka haraka kuudaka tena mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.
  Ibrahim Hajib alikaribia kuifungia Simba SC mara mbili dakika ya 18 na 32, lakini kali zaidi ilikuwa dakika ya 32 alipopiga mpira uliomshinda Kiiza, lakini ukatoka nje sentimita chache.
  Hamisi Kiiza akikimbia kushangilia bao lake la kwanza 
  Kiiza akifunga bao la kwanza dhidi ya Kagera Sugar leo
  Peter Mwalyanzi wa Simba SC kulia akiambaa na mpira
  Ibrahim Hajib wa Simba SC (kulia) akiambaa na mpira dhidi ya wachezaji wa Kagera Sugar, George Kavilla na Salum Kanoni
  Mashabiki wa Simba SC wakifurahia leo Uwanja wa Taifa

  Kipindi cha pili, nyota ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Kiiza ‘Diego’ iliendelea kung’ara baada ya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 46 akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. 
  Kagera Sugar walipata bao lao dakika ya 50 kupitia kwa Mbaraka Yussuf aliyetumia mwanya wa mabeki wa Simba SC kujichanganya. 
  Kiiza akakamilisha hat trick yake dakika ya 90 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya kiungo Mwinyi Kazimoto Mwitula na wachezaji karibu wote wa SImba SC wakaenda kucheza ‘mayenu’ mbele ya mashabiki wachache wa Yanga SC waliojitokeza Taifa leo.
  Mahasimu, Simba inayofundishwa na Muingereza Dylan Kerr na Yanga ya Mholanzi, Hans van der Pluijm watamenyana Septemba 26 katika mfululizo wa Ligi Kuu, timu zote zikitoka kushinda mechi tatu za awali.
  Yanga imezifunga Coastal Union 2-0, Prisons 3-0 na JKT Ruvu 4-1 jana, wakati Simba SC imezifunga 1-0 African Sports, 2-0 Mgambo na leo 3-1 Kagera Sugar. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Emery Nimubona/Hassan Kessy dk60, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Justuce Majabvi, Awadh Juma, Simon Sserunkuma/Pape Abdoulaye N’daw dk60, Said Ndemla, Ibrahim Hajib/Mwinyi Kazimoto dk81, Hamisi Kiiza na Peter Mwalyanzi.
  Kagera Sugar; Agathon Anthony, Salum Kanoni, Said Hassan/Abubakar Mtiro dk77, Ibrahim Job, Deogratius Julius, George Kavilla, Iddi Kurachi/Kenneth Masumbuko dk46, Lawrence Mugia/Babuu Ally dk30, Mbaraka Yussuf, Daudi Jumanne na Paul Ngalyoma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SALAMU ZAO JANGWANI…KIIZA APIGA HAT-TRICK SIMBA YAITANDIKA KAGERA SUGAR 3-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top