• HABARI MPYA

    Monday, June 01, 2015

    UNA RAMBO? MI NNA MUWA! YAMOTO BAND ‘SHIKENI ADABU ZENU’

    MJINI bana lisingie neno mbona tutakoma, sasa hivi kila mtu utamsikia “Una Rambo?” watoto wadogo ndio kabisaaa …Una Rambo? Mi nna muwa, ni ujinga ujinga tu mi hujaniua.
    Yamoto Band ni kundi linaloundwa na waimbaji wanne chipukizi lakini wenye uwezo wa hali ya juu, uwezo ambao umeifanya bendi hiyo iwe gumzo kila kona ya Tanzania na hata nje ya mipaka ya Bongo.
    Yupo mtu anaitwa Dogo Asylay, kuna Maromboso, yupo pia Beka Fleva bila kumsahau Enock Bella ambaye anatesa na sauti lake zito …Una Rambo? 
    Hao ndio madogo wanaounda kundi la Yamoto chini ya taasisi ya Mkubwa na Wanawe inayoongozwa na Said Fela.
    Nyimbo zao zote ni moto chini, hakuna ngoma yao ambayo haijatesa na kwasasa gumzo kubwa juu yao ni wimbo “Nitakupwerepweta” ambao umepokewa kwa hisia tofauti – wengine wakisema umejaa matusi, wengine wakisema uko poa na wako waliokwenda mbali zaidi kwa kutaka wimbo huo usipigwe hata kwenye vituo vya radio au luningani. 
    Mama mmoja alimsikia mwanae anaimba wimbo huo mbona ilikuwa ‘soo’ bi mkubwa akamkoromea mtoto na kumwambia: “Wewe na Yamoto yako shikeni adabu zenu, kaimbie huko huko, hapa kwangu usithubutu tena”
    Nimeusikiliza kwa makini sana wimbo huu, nikaurudia tena na tena, nakiri kabisa sijaona ubaya wa wimbo huo ambao kwa asilimia 90 umejaa maonyo ya gonjwa la hatari la UKIMWI.
    Narudisha nyuma sana fikra zangu na kuukumbuka wimbo wa marehemu Dr Remmy Ongala “Mambo kwa soksi” ambao ulipigwa marufuku lakini leo hii matangazo ya kondom tena yaliyojaa ushawishi wa ngono yametapakaa kila kona.
    Ukiufuatilia kwa makini wimbo huo wa Yamoto Band utagundua kuwa wengi wanakerwa na neno “Nitakupwerepweta” ambalo linamaanisha kupwaya au kutoenea – wameunda tafsiri mbovu wanavyojua wao ili tu kupotosha maana ya wimbo.
    Hebu tazama kipande hiki cha wimbo huo: “Unajifanya bingwa wa kupenda, kumbe bingwa wa kutenda kuliko kupenda, tena una sifa ya kuogopwa kama difenda, umeua wengi ila kwangu umedunda, usitake nizikwe na kilo mbili kwenye mfuko, usitake familia ilie kwa sababu yako, ananitegemea mama …nikifa atalia sana, katika familia nami ni baba japo baba yupo, nikija kufa ufa nani ataziba”.
    Angalia na kipande hiki: “Una kichaa mi nakuitaga mwendawazimu, nimepata habari mwili wako umeujaza sumu, unang’ang’ang’ana unataka mi kunipa utamu, umekosa singeli ngoma ya kucheza huna nenda kalicheze segere ….”
    Halafu endelea na kipande hiki: “Mimi si ‘size’ yako nitakupwerepweta bure, tafuta ‘type’ yako wa Ilala mimi wa Kilungule”. 
    Hayo ni baadhi tu ya maneno yenye akili yaliyojaa kwenye wimbo huo “Nitakupwerepweta” ambao watu flani wala hawayaoni.
    Wapi walipoharibu hawa madogo? Wapi walipokesea? Hakuna, sioni chochote zaidi ya kushuhudia ubunifu wa hali ya juu na wa kipekee ..Ni bonge la wimbo ambao kila kipande chake kina utamu wake.
    Hata wimbo wao “Niseme Nisiseme” nao ulikumbwa na shutuma kama hizo lakini ukiusikiliza kwa makini utagundua kuwa waligusa kabisa kwenye matukio mengi yanayotokea kila siku kwenye nyumba zetu … Najiuliza Yamoto washike adabu zao kwa kipi? Hebu tuwaache vijana watupe mautamu na elimu kupitia ubunifu wao wa aina yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UNA RAMBO? MI NNA MUWA! YAMOTO BAND ‘SHIKENI ADABU ZENU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top