• HABARI MPYA

    Saturday, June 13, 2015

    MSHAMBULIAJI WA SIMBA SC ATUA PRIMEIRO DE AGOSTO

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba SC, Selemani Yamin Ndikumana jana amesaini Mkataba wa mwaka mmoja na nusu kujiunga na klabu ya Primeiro de Agosto ya Angola. 
    Mpachika mabao huyo aliyezaliwa Machi 18, mwaka 1987 ametua klabu hiyo ya mjini Luanda, akitokea KF Tirana ya Albania.
    “Nimefurahi sana kutua hii timu kubwa ya jeshi hapa Angola. Niko tayari kwa changamoto mpya na nitazidisha bidii nitimize ndoto zangu, kutwaa mataji hapa,”amesema Ndikumana akizungumza na BIN ZUBEIRY leo kutoka Angola.
    Ndikumana amesema ameshindwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Burundi, ambacho leo kinamenyana na wenyeji, Senegal Uwanja wa Leopold Sedar Senghor mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa sababu ya dili hilo.
    “Nililazimika kuiacha timu ya taifa kuja kuwahi kusaini huku kabla ya dirisha lao la usajili halijafungwa leo,”amesema mshambuliaji huyo mwenye nguvu. 
    Ikumbukwe, Ndikumana aliibukia Inter Star ya kwao, Burundi kabla ya mwaka 2006 kujiunga na Simba SC ya Dar es Salaam.
    Januari mwaka 2008 Simba SC ilimuuza Molde FK ya Norway ambako alicheza hadi Desemba 8 mwaka huo huo, aliposaini Mkataba wa mwaka mmoja na Nusu na Lierse S.K. ya Ubelgiji ikiwa Daraja la Pili.
    Mwaka 2010 akarejea nyumbani Burundi kuichezea Fantastique ya Bujumbura baada ya kumaliza Mkataba wake Lierse S.K. kabla ya Januari mwaka 2013 kuibuka upya na kusajiliwa na El-Merrikh SC ya Sudan.
    Januari 31 mwaka 2014 akahamia KF Tirana ya Albania kabla ya jana kuhamia Primeiro de Agosto. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSHAMBULIAJI WA SIMBA SC ATUA PRIMEIRO DE AGOSTO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top