• HABARI MPYA

  Monday, January 22, 2018

  KAITABA LEO NI KIMBEMBE KAGERA NA SIMBA…NYOSSO NA BOCCO USO KWA USO TENA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MZUNGUKO wa 14 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unakamilishwa leo kwa mechi mbili Nyanda za Kuu Kusini na Kanda ya Ziwa Victoria.
  Mjini Bukoba mkoani Kagera, ukanda wa ziwa Victoria, wenyeji Kagera Sugar watawakaribisha Simba SC Uwanja wa Kaitaba na Uwanja wa Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma, wenyeji Maji Maji watawakaribisha Singida United.
  Mechi ya Bukoba imeteka hisia za wengi ikichukuliwa kama marudio ya mechi ya Jumapili ya Aprili 2, 2017 msimu uliopita ambayo Kagera Sugar walishinda 2-1 na kuitibulia Simba kutwaa ubingwa – hata Wekundu wa Msimbazi wakakata rufaa wakidai beki Mohammed Fakhi alicheza akiwa ana kadi tatu za njano.
  Rufaa hiyo iligonga besela Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kamati zake zote na Simba wakadai wamehamishia malalamiko yao FIFA, ingawa hadi leo hakuna mrejesho.
  Lakini pia, kukutana kwa wachezaji wawili uwanjani leo, beki Juma Said Nyosso wa Kagera Sugar na mshambuliaji John Raphael Bocco wa Simba kunatengeneza mvuto wa kipekee katika mechi hiyo.  
  Wote wakiwa Manahodha wa timu zao, Septemba 27, mwaka 2015 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Nyosso akiwa anachezea Mbeya City alimtomasa nyuma Bocco wa Azam FC na refa Martin Saanya hakuona hadi Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Ligi Kuu ilipokuja kumfungia miaka miwili na kumtoza faini ya Sh. Milioni 2 Septemba 30, 2015 kwa ushahidi wa picha.
  Baada ya miaka miwili, Nyosso atakayecheza dhidi ya timu yake ya zamani leo, Simba SC atakutana tena na Bocco wote wakiwa timu tofauti. Hakuna namna Bocco na Nyosso watakwepana kukabiliana uwanjani leo ikiwa watapangwa, kwani mmoja sentahafu na mwingine fowadi.
  Juma Nyosso akimtomasa nyuma John Bocco Septemba 27, mwaka 2015 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam huku refa Martin Saanya akiwa bize na mambo mengine  

  Uhondo zaidi katika mchezo wa leo ni mlinda mlango Juma Kaseja ambaye baada ya takriban muongo mmoja wa kuichezea Simba kwa mafanikio, leo atataka kuendelea kuikumbushia ubora wake timu yake ya zamani. 
  Simba wanaingia kwenye mchezo wa leo wakitoka kushinda 4-0 dhidi ya Singida United, wakati Kagera imecheza mechi tatu mfululizo bila kushinda, ikiwemo iliyopita waliyofungwa 1-0 na Njombe Mji FC Januari 15, baada ya sare mbili mfululizo za 0-0 na Stand United mjini Shinyanga na Mbeya City mjini Mbeya.
  Mara ya mwisho Kagera Sugar ilishinda Novemba 19, mwaka jana tena ugenini kwa ndugu zao, Mtibwa Sugar 1-0 Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro.
  Mjini Songea kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm leo atajaribu kupooza machungu ya kipigo 4-0 kutoka kwa Simba katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu mbele ya timu ngumu kufungika nyumbani, Maji Maji. Mechi zote kama kawaida zitaonyeshwa na Televisheni ya Azam TV kuanzia Saa 10:00 jioni.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAITABA LEO NI KIMBEMBE KAGERA NA SIMBA…NYOSSO NA BOCCO USO KWA USO TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top