• HABARI MPYA

    Sunday, November 19, 2017

    MSUVA ASIFU UTEUZI WA KIKOSI CHA BARA CHALLENGE, AKITABIRIA UBINGWA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva amepongeza uteuzi wa kikosi cha Bara katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu nchini Kenya.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo kwa simu kutoka Morocco anakochezea klabu ya Difaa Hassan El-Jadida, Msuva amesema  amempongeza kocha Ammy Ninje kwa uteuzi wa kikosi kizuri ambacho anaamini kinaweza kubeba Kombe la Challenge.
    “Ni Kikosi kizuri na kina baadhi ya wachezaji ambao hawajawahi kuitwa kabla kama Dani (Lyanga) na wengineo,”amesema Msuva, mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam.
    Simon Msuva amepongeza uteuzi wa kikosi cha Tanzania Bara kwenye Kombe la Challenge 

    Msuva amesema anaamini kikosi hicho kinaweza kufanya vyema kwenye michuano ya Challenge kama kitaata maandalizi mazuri; “Mimi naamini juu ya umoja na kumsikiliza mwalimu na viongozi wanasema nini au wanataka nini, ndivyo vitaleta mafanikio,” amesema.
    Ninje ameita makipa wawili tu katika kikosi cha wachezaji 20 alioteua ambao ni Aishi Manula wa Simba na Peter Manyika wa Singida United.  
    Mabeki ni Boniphace Maganga wa Mbao FC, Gardiel Michael, Kelvin Yondani wote wa Yanga, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ wote wa Simba na Kennedy Wilson wa Singida United.
    Viungo ni Himid Mao wa Azam FC, Hamisi Abdallah wa Sony Sugar ya Kenya, Raphael Daudi, Ibrahim Ajib wote wa Yanga, Muzamil Yassin, Jonas Mkude, Shiza Kichuya wote wa Simba na Abdul Hilal wa Tusker ya Kenya, wakati washambuliaji ni Mbaraka Yusuph wa Azam FC, Daniel Lyanga wa Fanja ya Oman, Elias Maguri na Yohana Nkomola wote huru.
    Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya, wakati Kundi B lina timu za Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.
    Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.
    Kili Stars itarudi uwanjani Desemba 7 kumenyana na Zanzibar Heroes, Desemba 9  na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya Desemba 11.
    Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Desemba 12 na Nusu Fainali zitachezwa Desemba 14 na 15, wakati Desemba 16 itachezwa mechi ya kusaka mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA ASIFU UTEUZI WA KIKOSI CHA BARA CHALLENGE, AKITABIRIA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top