• HABARI MPYA

  Monday, November 13, 2017

  LULU AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MIWILI JELA KIFO CHA KANUMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imemhukumu kifungo cha miaka miwili, mwigizaji wa kike, Elizabeth Michael ‘Lulu’ baada ya kukutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba.
  Akisoma hukumu hiyo leo, Jaji Sam Rumanyika amesema kwamba ushahidi wa mazingira umemtia kwenye hatia ya kuua msanii huyo, hivyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
  Lulu alidaiwa kumuua Kanumba Aprili 7, mwaka 2012 eneo la Sinza, Vatican mjini Dar es Salaam.

  UTETEZI WA LULU
  Katika utetezi wake, Lulu aliiambia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mwezi uliopita kwamba Kanumba alikuwa akilewa na kumpiga na kwamba Kanumba aliwahi alimpiga kwa panga mapajani na akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala.
  “Sijasababisha kifo cha Kanumba kwa namna yoyote ile. Umbo langu lilikuwa dogo hivyo mimi ndiyo nilikuwa nashambuliwa. Kama marehemu asingeanguka labda angenidhuru. Kanumba alikuwa kama mlezi wangu, tulianza mahusiano miezi minne kabla ya kifo chake,” amesema Lulu.
  “Nilikuwa nataka kutoka ila marehemu (Kanumba) alinikataza, alikuwa hataki nitoke, nilipomwambia natoka na marafiki zangu alinikimbiza na taulo na mimi nilikuwa naogopa kupigwa, mara nyingi alikuwa ananipiga kila akilewa na sio kwa akili zake.  Alipoona simu yangu inaita akahisi ni simu ya mwanaume akasema kwa nini naongea na simu ya mwanaume mbele yake? Marehemu akaingia uvunguni akatoa panga akasema leo nakuua huku akinipiga na panga kwenye mapaja”, ameelezea Lulu.
  Lulu ameendelea kusimulia…. “Marehemu alianguka mwenyewe na kujigonga kwa nguvu na kuinuka akitapatapa, nilimwambia Seth kuwa Kanumba amedondoka na akajaribu kumuamsha hakuamka,  akasema anaenda kumuita daktari, alivyosema anaenda kumuita daktari na mimi nikaondoka nikiogopa anaweza akaamka akaanza kunipiga.  Niliondoka nikawasha gari kuelekea Coco Beach kutuliza akili”.
  Muigizaji huyo ameendelea kusimulia kwamba … “Nilivyofika Coco Beach meseji zilianza kusambaa kuniuliza kuwa nasikia Kanumba amefariki, nikampigia Kidume ambaye ni rafiki yake Kanumba kumuuliza Kanumba yupo hospitali gani niende kumuona, akaniambia wewe usije hospitali, niambie uko wapi, tukakubaliana tuonane Bamaga.  Tulivyokutana Bamaga alikuwa kama anataka kuongea na mimi ghafla wakaja askari kunikamata,” ameeleza Lulu.
  Baada ya Muigizaji, Elizabeth Michael ‘Lulu’kuanza kujitetea katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar, kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Steven Kanumba bila kukusudia, msanii huyo amekana kuhusika na kifo hicho.
  Lulu ameeleza siku ya tukio, Kanumba alikuwa amelewa na yeye Lulu alitaka kutoka na marafiki zake lakini alimkataza, baada ya Kanumba kuona simu ya Lulu imeita alizani anaongea na mwanamme mwingine huku ambapo alichukua panga na kumkimbiza nalo. Kanumba alianguka na Lulu kuchukua gari na kukimbilia Coco Beach ambapo baadaye alikamatwa na Polisi maeneo ya Bamaga.
  Utetezi wa Lulu haupishani sana na ushahidi ndugu wa marehemu Steven Kanumba, Seth Bosco, ambaye aliisimulia mahakama jinsi ilivyokuwa siku ya tukio.
  Bosco alisema kwamba aligundua kuwa kaka yake hapumui baada ya kugombana na mpenzi wake Lulu.
  “Siku ya tukio marehemu Kanumba alinambia nisitoke nyumbani anataka tutoke wote kuanzia saa sita usiku, akaja Lulu na Kanumba ndiye aliyemfungulia mlango Lulu, alipofika ndani nikasikia akimuuliza Lulu kwanini anaongea na boyfriend wake mbele yake? Katika malumbano yao Kanumba alikuwa akimvuta Lulu arudi ndani na Lulu naye alikuwa anataka kutoka nje, wakati wakiendelea kugombana mlango wa chumba changu sikuufunga”, alisikika Seth akiisimulia Mahakama.
  Seth aliendelea kusimulia kuwa …..”Baada ya ugomvi Lulu alikuja chumbani kwangu akilia, akanambia Kanumba kadondoka amejaribu kummwagia maji haamki. Na ilikuwa mara ya kwanza kuona ugomvi kati yao, nilipoingia chumbani nilimkuta Kanumba chini kaegemea ukuta nikamlaza chali nikamtafuta daktari wake, Dk Kageiya, alipofika alimfanyia chek up akanambia ameshafariki ila akashauri tumpeleke hospitali ya Muhimbili”.
  Steven Kanumba enzi za uhai wake
  WASIFU WA LULU
  Elizabeth Michael 'Lulu' alizaliwa na kukulia Jijini Dar es Salaam, kwa baba Michael Kimemeta na mama Lucrecia Kalugira. 
  Alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Remnant Academy kabla ya kwenda sekondari za Perfect Vision na St Mary's, zote za Dar es Salaam.
  Kutoka hapo alijiunga na Chuo cha Utumishi wa Uma (TPSC), Magogoni, Dar es Salaam kwa masomo ya Stashahada ya Uongozi wa Rasilimali Watu (HRM).
  Wakati wote huo, Lulu tayari ni msanii maarufu tangu anasoma shule ya msingi akianzia kundi la Kaole lililokuwa na maskani yake Magomeni mjini Dar es Salaam kama mwigizaji mtoto mdogo.
  Mafanikio yake katika sanaa ni pamoja na ushindi wa tuzo ya Mwigizaji Bora wa Tamasha la Kimataifa la Filamu Tanzania (ZIFF) mwaka 2013 na tuzo ya Africa magic ya Filamu Bora Afrika Mashariki mwaka 2016.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LULU AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MIWILI JELA KIFO CHA KANUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top