• HABARI MPYA

    Monday, November 20, 2017

    KOCHA MRUNDI WA MBEYA CITY AKUBALI LAWAMA KIPIGO CHA JANA

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mrundi Ramadhani Nsanzurwimo (pichani kulia) amesema kwamba anastahili lawama kwa kipigo cha 5-0 kutoka kwa Yanga jana.
    Mbeya City jana ilichapwa 5-0 na mabingwa watetezi, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Mzambia Obrey Chirwa akifunga mabao matatu na mzawa, Emmanuel Martin akifunga mawili. 
    Akizungumza na Waandishi wa Habari jana baada ya mchezo huo, kocha Ramadhani alisema kwamba amesikitishwa mno na matokeo hayo, kwani ni kinyume kabisa matarajio yake.
    “Tulikuja na mipango ya kushinda hii mechi, lakini tumeshindwa  kufanikisha mipango yetu na matokeo yake tumefungwa sisi, imeniumiza sana. Ila ndiyo mchezo,”alisema.
    Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi amesema kwamba yeye ndiye anastahili kubeba lawama za kupoteza mchezo huo, lakini anakwenda kufanyia kazi mapungufu. 
    Kipigo hicho cha jana ambacho ni cha tatu mfululizo ikitoka kufungwa 1-0 mara mbili, na Azam FC mjini Dar es Salaam na Simba mjini Mbeya, kinaifanya Mbeya City ibaki na pointi zake 11 baada ya mechi 10 katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sawa na Maji Maji walio nafasi ya nane.
    Mbeya City itateremka tena uwanjani Ijumaa wiki hii kumenyana na wenyeji, Singida United Uwanja wa Namfua.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MRUNDI WA MBEYA CITY AKUBALI LAWAMA KIPIGO CHA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top