• HABARI MPYA

    Friday, January 15, 2016

    YANGA SC, AZAM FC ZAREJEA VITANI MBIO ZA UBINGWA LIGI KUU BARA, SIMBA YA MAYANJA…

    RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA;
    Januari 16, 2016
    Azam FC Vs African Sports
    Simba SC Vs Mtibwa Sugar
    JKT Ruvu Vs Mgambo JKT
    Toto Africans Vs Prisons
    Stand United Vs Kagera Sugar
    Mbeya City Vs Mwadui FC
    Coastal Union Vs Majimaji
    Januari 17, 2016
    Yanga SC Vs Ndanda FC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho, vinara Azam FC wakiikaribisha African Sports Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
    Azam FC iliyo kileleni mwa Ligi Kuu kwa pointi zake 35 baada ya kucheza mechi 13, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 33 za mechi 13 pia, imepania kushinda mechi hiyo ili kuzidi kupiga kasi katika mbio za ubingwa.
    Baada tu ya kutolewa katika Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar wiki iliyopita, Azam FC ilirejea Dar es Salaam mapema kuanza maandalizi ya mechi dhidi ya Sports.
    Na katika kipindi hiki kifupi wamefanya hadi mazoezi ya ufukweni kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa fiti kikamilifu.  
    Mechi nyingine za Ligi Kuu kesho ni baina ya mabingwa wa zamani wa ligi hiyo, Simba SC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu, watakutana Jumamosi ikiwa ni wiki moja tangu wakutane katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Mtibwa Sugar ikiilaza Simba SC 1-0, bao pekee la Ibrahim Rajab ‘Jeba’.
    Na baada ya kipigo hicho, Simba SC iliwafukuza makocha wake, Muingereza, Dylan Kerr na Mkenya Iddi Salim na sasa Mganda, Jackson Mayanja ndiye yupo na timu.
    Simba SC ilirejea Dar es Salaam jana mchana kwa maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa tena Mtibwa Sugar kesho katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
    Lakini Mtibwa Sugar nao wataingia katika mchezo wa kesho wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-1 na URA ya Uganda katika fainali ya Kombe la Mapinduzi juzi. 
    Mechi nyingine za ligi hiyo kesho ni kati ya JKT Ruvu na Mgambo JKT Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, Toto Africans na Prisons Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Stand United na Kagera Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mbeya City na Mwadui FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Coastal Union na Majimaji wa Uwanja wa Majimaji, Songea.
    Ligi Kuu itaendelea Jumapili kwa mechi moja tu, mabingwa watetezi, Yanga SCwakiikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga SC nayo inarejea kwenye Ligi Kuu baada ya kutolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, wakifungwa kwa penalti 4-3 na URA kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC, AZAM FC ZAREJEA VITANI MBIO ZA UBINGWA LIGI KUU BARA, SIMBA YA MAYANJA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top