• HABARI MPYA

    Friday, January 15, 2016

    MOISE KATUMBI HATAKI KUMUUZA SAMATTA UBELGIJI, ANATAKA AENDE NANTES YA UFARANSA NA YUKO TAYARI DILI LIFE ABAKI MAZEMBE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKATI tayari amepatiwa viza na Ubalozi wa Ubelgiji kwenda kusaini klabu ya KRC Genk, mshambuliaji Mbwana Ally Samatta anaweza akabaki TP Mazembe ya DRC kumalizia Mkataba wake hadi Aprili.
    Hiyo inatokana na Rais wa Mazembe, Moise Katumbi kugoma kumuuza Mwanasoka huyo Bora Anayecheza Afrika katika klabu hiyo Ligi Kuu ya Ubelgiji.
    BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu Katumbi anataka Samatta aende Nantes FC ya Ligi Kuu ya Ufaransa, ambayo amekwishafikia makubaliano nayo, 
    na wiki iliyopita Nantes FC ilituma mwakilishi wake Dar es Salaam, ambaye alifanya mazungumzo na Meneja wa Samatta, Jamal Kisongo mbele ya Ofisa mmoja wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Samatta sasa anatarajia msaada wa Serikali kumlainisha Moise Katumbi akubali kupokea ofa ya KRC Genk

    Na katika mazungumzo, Kisongo alifikia makubaliano ya maslahi binafsi na Samatta ikiwemo dau la kusaini, mshahara, masharti na marupurupu mengine.
    Kisongo alitaka kiwepo kipengele cha mchezaji kutorejeshwa Afrika iwapo hatapata nafasi ya kucheza Nantes, bali auzwe klabu nyingine ya Ulaya na ikakubaliwa.
    Nantes ilionyesha nia ya dhati kabisa ya kumchukua Samatta na Kisongo aliinuka kwenye meza ya mazungumzo akiwa amekubali na kusema anakwenda kuzungumza na mchezaji.
    Hata hivyo, inaonekana Samatta mwenyewe ndiye anayetaka kwenda Ubelgiji na si Ufaransa, kwani kitendo cha Kisongo kutorejesha majibu kwa Nantes kinaashiria ameshindwa kumshawishi mchezaji wake akubali ofa hiyo.
    Wakati huo huo, Rais wa Mazembe hayuko tayari kumuuza Samatta Ubelgiji na yuko tayari kuona Samatta anabaki Mazembe kumalizia Mkataba wake ili aondoke kama mchezaji huru Aprili, hali ambayo itamlazimu kusubiri hadi Agosti kusaini Genk.
    Kwa sasa, kambi ya Samatta inajaribu kuomba msaada kwa viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakazungumze na Katumbi ili akubali kumuacha mchezaji aende klabu aliyochagua.
    Rais Mstaafu, Dk Jakaya Mrisho Kikwete ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama tawala, CCM, Waziri wa Michezo, Nape Nnauye kwa pamoja wameahidi kumsaidia Samatta katika suala la kumlainisha katumbi akubali kupokea ofay a Genk.
    Moise Katumbi anataka Samatta aende Nantes ya Ufaransa

    Wakati huo huo, Nantes wamekuwa wakimpigia simu Kisongo wakisema wanamsubiri mchezaji aende kusaini, lakini Meneja huyo anakosa majibu ya uhakika.
    Inaonekana tayari Katumbi anaujua mchezo wote unaoendelea naye ameamua kukaa kimya akiamini Samatta hawezi kufanya chochote kwa sasa bila baraka zake. 
    Na wazo la kusema Samatta asubuhi hadi Aprili atakapomaliza Mkataba wake ili asubiri kusaini kama mchezaji huru Agosti halifurahiwi hata na Kisongo mwenyewe.
    Samatta aliyejiunga na TPM mwaka 2011 akitokea Simba SC aliyoichezea kwa nusu msimu, akitokea African Lyon, hadi sasa ameichezea klabu hiyo mechi 103 na kuifungia mabao 60.
    Ndani ya mechi hizo, kijana huyo wa umri wa miaka 24, ameshinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na Mazembe, huku naye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MOISE KATUMBI HATAKI KUMUUZA SAMATTA UBELGIJI, ANATAKA AENDE NANTES YA UFARANSA NA YUKO TAYARI DILI LIFE ABAKI MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top