• HABARI MPYA

    Wednesday, March 29, 2023

    SI MUDA WA KULAUMIANA, TUJIPANGE KWA MECHI ZIJAZO

    TANZANIA jana imejiweka pagumu tena kwenye mchuano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kuchapwa 1-0 na Uganda Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Kundi F.  
    Bao pekee la The Cranes lililoizamisha Taifa Stars jana lilifungwa na winga, Rogers Mato Kassim wa KCCA ya nyumbani, Kampala dakika ya 90 na ushei akimalizia kazi nzuri ya Farouk Miya wa Rizespor ya Uturuki.
    Sasa msimamo wa Kundi F ni; Algeria imekwishafuzu ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na Tanzania na Uganda zenye pointi nne kila moja, wakati Niger ina pointi mbili baada ya timu zote kucheza mechi nne.
    Taifa Stars iliingia kwenye mchezo wa jana ikiwa na matumaini makubwa ya kushinda kufuatia kuwafunga 1-0 Uganda, bao pekee la mshambuliaji wa Al Qadsiah ya Saudi Arabia, Simon Msuva kwenye mchezo wa Ijumaa iliyopita mjini Ismailia nchini Misri.


    Baada ya kipigo cha jana lawama zaidi amesukumiwa kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche ambaye alikuwa anaiongoza timu katika mchezo wa pili tu tangu aanze kazi.
    Amelaumiwa kwa mabadiliko aliyoyafanya kwenye kikosi kipindi cha pili kwa kuwatoa beki wa kushoto Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na viungo Himid Mao Mkami na Muzamil Yassin na kuwaingiza beki David Luhende, kiungo Feisal Salum na beki Shomari Kapombe – kwamba yaliidhoofisha timu hadi kuruhusu bao la dakika ya 90 na ushei la Uganda.
    Mara baada ya kupewa timu, Amrouche alipanga kikosi kisichotarajiwa kabisa kwenye mechi dhidi ya Uganda – ajabu zaidi akimuanzisha beki Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambaye alikuwa ameitwa kikosini kwa mara ya kwanza.
    Lakini hakuwaita mabeki wazoefu Shomari Kapombe na Tshabalala kwa ajili ya mechi ya kwanza na Uganda na akaenda kuwatumia beki wa kati Dickson Job kama beki wa kulia na kiungo Novatus Dissmas kama beki wa kushoto.
    Timu ilishinda ugenini na Mualgeria huyo akamwagiwa sifa za kutosha na kuelekea mechi ya jana Watanzania walikuwa wana matumaini makubwa na kocha huyo na timu pia.
    Kama ingeshinda jana, Taifa Stars ingepigania ushindi mwingine dhidi ya Niger ili kujihakikishia tiketi ya Ivory Coast mwakani.
    Watanzania wana kiu ya kucheza AFCON ya tatu kihistoria baada ya ile ya kwanza mwaka 1980 nchini Nigeria na ile mwaka 2019 nchini Misri, ambayo wachezaji wengi waliokuwemo kwenye kikosi hicho wapo kwenye kikosi cha sasa chini ya Nahodha Mbwana Samatta.    
    Lawama kwa kocha Amrouche siku chache tu tangu asifiwe – hiyo ndiyo rangi yetu halisi wa Tanzania. Tumekuwa watu wa kusukumwa na upepo.
    Ukiachilia mbali muda mdogo wa Amrouche kazini – lakini Watanzania wanapaswa kufahamu soka imebadilika mno kwa sasa barani Afrika na ili kupata mafanikio tunahitaji kuwekeza kwenye utengenezaji wa timu na si hamasa pekee.
    Kipigo cha jana kimewakumbusha Watanzania machungu ya Septemba 8 mwaka 2007 Taifa Stars ilipochapwa 1-0 na Msumbiji hapo hapo Uwanja wa Mkapa, wakati huo unajulikana kama Uwanja wa Taifa, bao pekee la ‘Manuel José Luís Bucuane’ Tico-Tico dakika ya nane.
    Ulikuwa mchezo wa mwisho wa Kundi la Saba kuwania tiketi ya AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana ambao Tanzania iliingia ikihitaji ushindi kufuzu japo kama mmoja wa washindi wa pili bora.
    Imetukumbusha pia namna ambavyo Taifa Stars ilitandikwa 3-0 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hapo hapo Mkapa Novemba 11 mwaka 2021 katika mchezo wa marudiano Kundi J kufuzu Kombe la Dunia mwaka jana Qatar.
    Stars iliingia kwenye mechi na DRC ikiwa na matumaini makubwa ya ushindi baada ya kulazimisha sare ya ugenini ya kufungana 1-1 Uwanja wa TP Mazembe mjini Lubumbashi katika mchezo ambao wenyeji walitangulia kwa bao la Dieumerci Mbokani dakika ya 23, wakati la wageni lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 36 na Msuva.
    Kwa wahenga imewakumbusha hadi Desemba 20, mwaka 1980 tulipochapwa 2-0, mabao ya John Okechukwu Chiedozie dakika ya tano na Christian M'Wokozhi dakika ya 79 Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) Jijini Dar es Salaam mechi ya Raundi ya Pili kufuzu Kombe la Dunia 1982.
    Taifa Stars ilifungwa 2-0 nyumbani ikitoka kutoa sare ya 1-1 ugenini, Desemba 6 1980, Super Eagles, wakati huo Green Eagles wakitangulia kwa bao la Mudashiru Babatunde "Muda" Lawal dakika ya 29 kabla ya beki Mohamed Salim kuisawazishia Tanzania dakika ya 85 Uwanja Surulere Jijini Lagos, Nigeria.
    Ni mfululizo wa matokeo ya aina hii yaliyowarudisha nyuma Watanzania kuisapoti timu yao, au timu zao taifa hadi kuelekea mchezo wa jana na Uganda zilihitajika hamasa kubwa ikiwemo mashabiki kuingia bure kwa tiketi zilizokatwa na viongozi wa nchi wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na wadau.
    Matokeo ya aina hii yaliwakatisha tamaa hata Marais wa Serikali zilizopita kuendelea kusaidia timu za taifa baada ya awali kujitolea ikiwemo kulipia makocha na kambi kama ambavyo imefanya Serikali ya rais Samia Suluhu Hassan.
    Tunakwenda kwenye mechi mbili za mwisho za Kundi F kufuzu AFCON ya mwakani nchini Ivory Coast, Juni 12 dhidi ya Niger hapa na Septemba 4 dhidi ya Algeria Jijini Algiers tukihitaji kushinda ili tuangalie nafasi yetu dhidi ya Uganda.
    Uganda wao watakuwa wenyeji wa Algeria Juni 12 kabla ya kuwafuata Niger Septemba 4 baada ya hapo waangalie hatma yao dhidi yetu. Kila hesabu zetu ni za kwao pia kwa sababu nafasi yetu ni kama wapo kadhalika.
    Kwa mantiki hiyo, huu si wakati wa kulaumiana, bali kwanza kuunganisha nguvu zetu kila mmoja kwa nafasi yake kuangalia namna ya kusaidia kampeni za Taifa Stars kufuzu AFCON ya mwakani nchini Ivory Coast. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SI MUDA WA KULAUMIANA, TUJIPANGE KWA MECHI ZIJAZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top