• HABARI MPYA

  Wednesday, March 22, 2023

  HII NDIYO MAANA HALISI YA KLABU KUJIENDESHA KIBIASHARA

  MARA tu baada ya kufanikiwa kufuzu Hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika Desemba mwaka jana, klabu ya Yanga iliingia mkataba na kampuni ya Haier wenye thamani ya Sh Bilioni 1.5.
  Haier ilichukua nafasi ya wadhamini wakuu wa Yanga, kampuni ya Sport Pesa kukaa kifuani mwa jezi za klabu hiyo kwenye mechi sita za Kombe la Shirikisho au zaidi kama wana Jangwani watasonga mbele.
  Tayari Yanga imefanikiwa kuingia Robo Fainali, maana yake Haier wana mechi mbili zaidi za kuendelea kujitangaza kifuani mwa jezi za klabu hiyo kupitia michuano ya CAF.
  Lakini inakumbukwa mara tu baada ya Yanga kuingia mkataba na Haier uliibuka mgogoro baina yao na wadhamini wao wakuu, SportPesa wakidai klabu hiyo imekiuka makubaliano kwa kuipa nafasi kampuni nyingine kifuani mwa jezi zao.


  Lakini Yanga ilitumia fursa ya SportPesa kutoruhusiwa na wenye mashindano yao, CAF kujitangaza kwenye jezi za klabu hiyo kama inavyofahamika tayari shirikisho hilo la soka barani lina mdhamini wa aina hiyo.
  Na Yanga walitumia weledi kuielewesha vyema tu Sport Pesa ambayo ilifikisha malalamiko yake hadi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kutishia kwenda hadi mahakamani kudai haki zaidi. Bila shaka walimalizana kikubwa na ndiyo maana mgogoro huo uliisha kimya kimya.
  Sifa ziende kwa uongozi wa Yanga chini ya Rais wake, Injinia Hersi Said na Mtendaji Mkuu, Mzambia, Adre Mtine kwa kufikiri haraka na kutumia fursa hiyo kuiongezea pato klabu, jambo ambalo wazi limeongeza ufanisi katika uendeshaji wa timu.
  Bila kuhusisha mapato ya mlangoni kwenye mechi zake tatu za nyumbani – Yanga tayari ilikuwa ina Sh. Bilioni 1.5 kwa sababu ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika pekee kutoka Haier.
  Na pamoja bonasi za wadhamini wa michuano hiyo dola za Kimarekani 350,000 (Sh. 818,999978.65) kwa kufika Robo Fainali tu – hapana shaka Yanga imefanya biashara nzuri hadi sasa tangu Desemba tu.
  Klabu zetu zinahitaji viongozi weledi kama hawa wa Yanga ya sasa wenye kufikiri na kuamua kwa usahihi na kwa haraka ili kwenda na wakati – maana yake kuna msemo maarufu sasa kwamba; Mambo mengi muda mchache. Hongera viongozi Yanga. 
  Hii ndiyo maana halisi ya klabu kujiendesha kibiashara. Ni mchezo wa kuingiza fedha zaidi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HII NDIYO MAANA HALISI YA KLABU KUJIENDESHA KIBIASHARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top