• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 12, 2020

  TFF YABAINI MKATABA WA MORRISON YANGA SC ULIKUWA NA UTATA, ARUHUSIWA KWENDA SIMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemtangaza winga Mghana, Bernard Morrison kuwa mchezaji huru baada ya kubaini mkataba wake na klabu ya Yanga ulikuwa una mapungufu.
  Baada ya shauri lililosikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia juzi, hatimaye leo jioni Mwenyekiti Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Wakili Elias Mwanjala amesema; 
  “Malalamiko, kesi iliyoletwa kwetu na Bernard Morrison kusema kwamba yeye hakusaini mkataba wa wa kuongeza muda na Yanga, kwa hiyo tumeangalia vitu vingi, kimsingi tumegundua kwamba mkataba una walakini kidogo, kwa hiyo tumempa faida Morrison, kwa maana ya kwamba tumeona kwamba Yanga wana mkataba ambao ulikuwa una utata kidogo,”.


  Pamoja na hayo, Wakili Mwanjala amemuagiza Morrison arejeshe fedha dola za Kimarekani 25,000 alizochukua Yanga SC kwa ajili ya mkataba huo wenye mapungufu.
  Na Mwanjala pia amesema Morrison atapelekwa Kamati ya Maadili kwa kitendo cha kusaini mkataba wa Simba wakati shauri lake halijatolewa hukumu.
  Morisson aliyejiunga na Yanga SC Januari mwaka huu kama mchezaji huru kwa mkataba wa miezi sita, alitambulishwa Simba SC Agosti 8 wakati hukumu yake awali ilitarajiwa kutolewa Jumatatu ya juzi.
  Baada ya mwanzo mzuri katika mkataba wake wa miezi sita Yanga SC, akifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi dhidi ya watani, Simba SC Machi 8 Uwanja wa Taifa, sasa Mkapa ikaripotiwa ameongezwa Morrison mkataba wa miaka miwili.
  Siku chache baadaye Morrison akaibuka akidai Simba wanamshawishi kujiunga nao kwa ofa nzuri zaidi na Yanga SC ikawasilisha malalamiko TFF dhidi ya mahasimu wao kukiuka taratibu za usajili. 
  Morrison akagoma kusafiri na Yanga SC Kanda ya Ziwa kabla ya kuibuka kwa taarifa anataka kuondoka kufuata ofa nzuri Uarabuni katika klabu ambayo hata hivyo hakuitaja.
  Tangu hapo mahusiano ya Yanga na mchezaji huyo yakazidi kuwa mabovu kiasi cha kuripotiwa hadi kumshikia kisu Meneja wa klabu, Abeid Mziba kambini, ingawa aliendelea kuitumikia klabu.  
  Morrison akafungua kesi TFF kupinga mkataba wa hadi 2022 akida yeye ana mkataba wa miezi sita tu ambao umemalizika Julai. TFF ilimuamuru Morrison kurejea kazini Yanga wakati shauri lake linaendelea kusikilizwa.
  Julai 12, mwaka huu Morrison akaondoka moja kwa moja baada ya kufanyiwa mabadiliko katika mchezo dhidi ya Simba SC Uwanja wa Taifa nafasi yake ikichukuliwa na Mnyarwanda Patrick Sibomana dakika ya 64 katika mchezo wa Nusu Fainali Kombe la TFF, maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC). 
  Tangu siku hiyo, Yanga ikachapwa mabao 4-1 Mghana huyo akicheza chini ya kiwango – hajaonekana tena kwenye kambi ya timu hiyo iliyomaliza Ligi Kuu katika nafasi ya pili nyuma ya mahasimu wao hao wa jadi, Smba SC.
  Morrison mwenye umri wa miaka 27, awali aliibukia klabu ya Heart of Lions mwaka 2013, kabla ya kuhamia Ashanti Gold mwaka 2015, zote za kwao Ghana.
  Mwaka 2016 alijiunga na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako alidumu hadi 2018 alipohamia Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
  Mwaka 2019 alirejea DRC kujiunga na DC Motema Pembe ambako alicheza kwa nusu msimu na kurejea kwao Ghana kabla ya kusajilwa Yanga SC Januari mwaka huu.
  Baada ya hukumu hiyo, Yanga SC imesema itakata Rufaa Mahakama ya Usuluhishi (CAS) ya Shrksho la Soka la Kimataifa (FFA), huku Smba wakitangaza mkutano na Waandishi wa Habari asubuhi ya kesho Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF YABAINI MKATABA WA MORRISON YANGA SC ULIKUWA NA UTATA, ARUHUSIWA KWENDA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top