• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 03, 2020

  KAMATI YA NIDHAMU YA TFF YAMFUNGIA EYMAEL MIAKA MIWILI NA KUMTOZA FAINI SH. MILIONI 8

  Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia aliyekuwa kocha wa Yanga SC, Mbelgiji, Luc Eymael miaka miwili na kumtoza faini ya jumla ya Sh. Milioni 8 kwa kosa la uchochezi na ubaguzi.
  Ni makosa hayo yalisababisha Eymael afukuzwe kazi Yanga SC mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya miezi saba tu kazini kutokana na kutoa kauli zilizotafsiriwa kama za kibaguzi dhidi ya mashabiki.
  Yanga ilisema kwamba kutokana na kauli hizo za kibaguzi uongozi umeamua kumfuta kazi Eymael kuanzia Julai 27, mwaka huu na kuhakikisha anaondoka nchini haraka iwezekanavyo.
  “Uongozi wa klabu ya Yanga umesikitishwa na kauli zisizo za kiungwana na za kibaguzi zilizotolewa na Kocha wake Luc Eymael na kusambaa katika mitandao ya kijamii,”ilisema taarifa ya Yanga na kuongeza;.
  “Baadhi ya kauli hizo za Kocha Luc Eymael amesikika akitoa kauli za kuwashutumu Mashabiki kwamba hawana elimu, watu kwenye nchi hii ni wapumbavu, mashabiki hawajui mpira kazi yao ni kupiga kelele kama nyani na bata, Viongozi wa Klabu ni sifuri na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya Simba tu,”.
  Aidha, Uongozi wa Yanga umewaomba radhi viongozi wa nchi, Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Viongozi wa Klabu ya Simba, wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga, pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kauli za kuudhi na kudhalilisha zilizotolewa na kocha huyo.
  “Klabu ya Yanga inathamini na kuamini katika misingi ya nidhamu na utu, na inapingana na aina yoyote ya Ubaguzi,”iliongeza taarifa hiyo iliyosainiwa na kaimu Katibu Mkuu wa klabu, Wakili Simon Patrick.
  Eymael ameondoka Yanga SC baada ya kuiongoza timu katika mechi 32 tangu ajiunge nayo Januari ikishinda 16, sare 11 na kufungwa tano akiiongoza kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ikizidiwa pointi 16 na mabingwa, Simba SC na wakiwazidi pointi mbili Azam FC waliomaliza nafasi ya tatu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAMATI YA NIDHAMU YA TFF YAMFUNGIA EYMAEL MIAKA MIWILI NA KUMTOZA FAINI SH. MILIONI 8 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top