• HABARI MPYA

  Thursday, January 09, 2020

  MTIBWA SUGAR YATANGULIA FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI BAADA YA KUITOA YANGA SC KWA MATUTA

  Na Saada Akida, ZANZIBAR
  TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa penalti 4-2 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Kipa wa tatu wa Yanga, Ramadhani Awam Kabwili alipangua penalti ya kiungo Abdulhalim Humud ‘Gaucho’, lakini wenzake beki Kelvin Yondani akagongesha mwamba na kiungo Abdulaziz Makame akapiga juu ya lango.
  Waliofunga penalti za Mtibwa Sugar ni Omary Sultan, Dickson Job, Jaffary Kibaya na Shomari Kibwana na za Yanga zilifungwa na beki Paul Godfrey ‘Boxer’ na kiungo Mapinduzi Balama ‘Kipenseli’. 
  Awali, Yanga SC ilitangulia kwa bao la kiungo wake mshambuliaji, Deus David Kaseke dakika ya 36 na Mtibwa Sugar ikasawazisha dakika ya 90 kupitia Shomari Kibwana.

  Nusu Fainali nyingine itafuatia kesho kwa mchezo baina ya mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC dhidi ya washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Azam FC Saa 2:15 usiku hapo hapo Uwanja wa Amaan, wakati fainali itafanyika Jumapili.  
  Mchezo wa leo ulishuhudiwa na kocha Mbelgiji, Luc Aymael aliyewasili Dar es Salaam leo kwa ajili ya kukamilisha mipango ya kujiunga na timu hiyo na moja kwa moja kwenda kuungana na timu visiwani Zanzibar.
  Luc Aymael anakuja Yanga baada ya kuzifundisha klabu za AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Missile ya Gabon, AFC Leopard ya Kenya, Rayon Sport ya Rwanda, JS Kairouan ya Tunisia, Al Nasr ya Dubai, Al Merreikh ya Sudan, Polokwane City, Free State Stars, Black Leopard za Afrika Kusini na Tala'ea El Gaish ya Misri.
  Kikosi cha Mtibwa Sugar kilikuwa; Said Mohammed ‘Nduda’, Dickson Job, Haruna Chanongo/Ally Makarani, Cassian Ponera, Riphat Khamis, Awadh Juma/Jaffary Kibaya, Salum Kihimbwa/Omary Sultan dk79, Awadh Salum, Issa Rashid, Abdulhalim Humud na Kibwana Shomari.
  Yanga SC: Ramadhani Kabwili, Paul Godfrey, Adeyum Saleh, Ally Ally, Andrew Vincent ‘Dante’, Said Juma ‘Makapu’, Deus Kaseke, Feisal Salum, Adam Stanley, Raphael Daud/Kelvin Yondani na Mapinduzi Balama.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  1 comments:

  Anonymous said... January 10, 2020 at 1:07 PM

  Kunyooshwa ni kunyooshwa tu iwe kwa mbinde au matuta, ukinyooshwa we kaa kimyaa sindano ikuiingie vizuri!

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YATANGULIA FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI BAADA YA KUITOA YANGA SC KWA MATUTA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top