• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 07, 2019

  WAMBURA AACHIWA HURU KWA SHARTI LA KULIPA SH MILIONI 100 BAADA YA KUKIRI ‘KUITAPELI’ TFF

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam leo imemuachia huru aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura kwa sharti la kulipa kiasi cha 100,998,121 kwa awamu tano.
  Na hiyo ilifuatia upande wa mashitaka kumfutia Wambura mashitaka ya uhujumu uchumi na kumsomea mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kosa ambalo alikiri kutenda.
  Hakimu mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina amesema kwamba mshitakiwa atatakiwa kulipa fedha hizo kwa awamu tano kuanzia leo ambapo alilipa Sh. Milioni 20 na kuachiwa huru.

  Wambura atatakiwa kulipa Sh 20,249,531 Desemba 31 na kiasi kingine kama hicho mwakani kuanzia Machi 31, Juni 30 na Septemba 30 na katika kipindi cha mwaka mzima ametakiwa kutofanya kosa lolote la jinai, ingawa rufaa ipo wazi kama hataridhika.
  Awali, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon alidai hawana rekodi ya makosa ya nyuma ya mshitakiwa huyo na kuiomba mahakama itoe adhabu kulingana na makubaliano, ili iwe fundisho kwake na wengine.
  Na Wambura akajitetea mahakamani hapo akisema hilo ni  kosa lake la kwanza kuomba asipewe adhabu itakayomnyima fursa ya kufanya shughuli nyingine za kijamii.
  Mapema akisoma makubaliano hayo, Wankyo alisema kwamba wamekubaliano na Wambura baada ya kukiri kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu aondolewe mashitaka ya kughushi, kutoa nyaraka za uongo na utakatishaji fedha ambayo ni mashitaka ya uhujumu uchumi na kulipa fedha zote kwa awamu tano.
  Hakimu Mhina alimuapisha Wambura na kumuuliza  kama alisaini kwa hiari yake ambapo alikiri kufanya hivyo kwa utashi wake.
  Akisoma mashitaka mapya, Wakili Simon alidai Julai 6, 2004 na Oktoba 30, 2015 maeneo ya Ilala Wambura alijipatia Sh 100,998,121 kwa udanganyifu kutoka TFF kwa lengo la kuonyesha malipo ya mkopo wa dola za Kimarekani 30,000 kutoka  Kampuni ya Jekc System Limited.
  Katika maelezo ya awali, Simon alidai Wambura kipindi hicho akiwa katibu Mtendaji wa TFF, Novemba 28,2002 waliingia makubaliano ya mkopo wa Dola za Marekani 30,000 lengo kufadhili michuano ya Chalenji kipindi hicho mwenyeji alikuwa Tanzania.
  Alidai Wambura alisaini makubaliano hayo kwa niaba ya TFF na kwamba walitakiwa kurudisha fedha zote pamoja na riba ya asilimia tano mara baada ya mashindano kukamilika.
  Alidai Januari 13,2014 Kampuni ya Jekc System Limited iliandika barua kwa mshitakiwa na kwa njia ya udanganyifu Wambura aliilaghai TFF kwa kujaribu kuonesha alichaguliwa na kupewa mamlaka ya kisheria kukusanya fedha hizo kwa niaba ya TFF.
  Wambura alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo akiwa na mashitaka 17 ikiwemo ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutoka nyaraka za uongo na utakatishaji fedha.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAMBURA AACHIWA HURU KWA SHARTI LA KULIPA SH MILIONI 100 BAADA YA KUKIRI ‘KUITAPELI’ TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top