• HABARI MPYA

    Sunday, September 11, 2016

    MALINZI AMLILIA SIANG'A, AWAPA POLE BUKOBA TETEMEKO LA ARDHI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kwamba limezipokea kwa masikitiko taarifa za kifo Kocha wa zamani wa Simba, James Aggrey Siang’a, aliyefariki juzi kwao Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu.
    Siang’a alikuwa ni miongoni mwa makocha walioheshimika Afrika Mashariki hususani Tanzania alipoingoza Simba kufanya vema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufika hatua ya timu Nane Bora.
    Kutokana na kifo hicho, Rais wa TFF Jamal Malinzi amemtumia salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa akieleza kwamba ameshtushwa na kifo cha Siang’a.
    Rais Malinzi mbali ya kutuma salamu FKF, pia alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Siang’a kadhalika ndugu, jamaa, majirani na marafiki huku akiwataka kuwa na moyo wa subira wakati huu mgumu wa msiba wa mpendwa wao.
    Rais Malinzi amesema kwamba Siang’a ameacha alama ya wadau wa soka kujifunza na kukumbukwa daima baada ya kucheza mpira wa miguu kwa mafanikio makubwa akichezea Klabu za Gor Mahia, Luo Union na timu ya taifa Kenya Harambee Stars kama kipa, pia aliwahi kuwa kocha wa klabu za Simba, Moro United na Express ya Uganda kama kocha.
    Kwa mujibu wa historia ya Siang’a aliidakia Kenya katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1972 na pia alikuwa kocha wa Harambee Stars mwaka 1999 na 2000, kabla ya kuhamia Tanzania kufundisha Simba, Mtibwa Sugar, Moro United na timu ya taifa ya Bara kwa muda mfupi mwaka 2002.
    Kwa Tanzania, atakumbukwa na familia nzima ya Simba kutokana na kuipa timu taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati visiwani Zanzibar mwaka 2002, kabla ya kuunda kikosi imara cha vijana wadogo kilichokuwa tishio katika soka ya Tanzania miaka 14 iliyopita wakiwamo Steven Mapunda ‘Garincha’, Said Swedi, Ramazani Wasso, Boniface Pawasa, Victor Costa, Lubigisa Madata, Suleiman Matola, Primus Kasonzo, Christopher Alex, Shekhan Rashid, Ulimboka Mwakingwe, Emmanuel Gabriel na Athumani Machuppa.
    Vijana hao ndio walioiwezesha Simba SC kuitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa wa Afrika katika hatua ya 16 Bora na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako awali walizitoa timu za BDF XI ya Botswana, Santos ya Afrika Kusini kabla ya Zamalek. Santos aliitoa kwa penalti 9-8 baada ya sare ya jumla 0-0 na Zamalek pia aliitoa kwa penaliti 3-2, baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Mzee Siang’a mahala pema peponi.
    Wakati huo huo: Malinzi ameshitushwa na taarifa za tukio la tetemeko kubwa ardhi lenye mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 lililotokea jana Septemba 10, 2016 katika mikoa mitatu ya Kanda ya Ziwa kadhalika nchi za Burundi na Uganda.
    Mikoa ya Kanda ya Ziwa iliyopata athari kwa mujibu wa taarifa ni Mwanza, Mara na Kagera nchini na kuripotiwa kuua zaidi ya watu 10 na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa sambamba na kubomoa majengo mbalimbali.
    Rais Malinzi mara moja anaungana na Serikali katika kusubiri tathmini na kisha kuangalia namna TFF itakavyoweza kusaidia kama sehemu ya wadau katika jamii. TFF inaamini kuwa baadhi ya waliopata maafa ni familia ya mpira wa miguu si ndani tu ya nchi, bali pia nje ya mipaka ya Tanzania.
    Hivyo, Rais Malinzi ametutuma salamu za rambirambi kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki na anawaombea marehemu wapumzishwe mahali pema peponi. Amina. Na amewaombea kwa Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
    Katika salamu hizo, pia Rais Malinzi amemtumia Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Burundi (BFF), Marlon Kuylen kwa sababu sehemu ya Bujumbura imeguswa na tetemeko hilo kadhalika ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Moses Magogo baada ya ripoti kuonesha kuwa tetemeko hilo limeukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda. Wataalamu wa elimu ya miamba – Jiolojia wanasema kwamba lilikuwa ni kubwa kwa mujibu wa vipimo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI AMLILIA SIANG'A, AWAPA POLE BUKOBA TETEMEKO LA ARDHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top