• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 29, 2016

  MO DEWJI ANAMWAGA FEDHA TU SIMBA...SASA MSIMBAZI NI BWAWA LA NEEMA!

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MFANYABIASHARA Mohamed 'Mo' Dewji sasa ndiye analipa mishahara ya wachezaji wa klabu ya Simba, kufuatia kujitoa kwa aliyekuwa mdhamini mkuu wa klabu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE  leo kwamba, klabu inamshukuru mlezi wake, Mo Dewji kwa kuanza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo.
  Manara amesema; "Dewji maarufu kama MO tayari ameshaanza kulipia mishahara ya wachezaji,benchi la ufundi na Sekretarieti ya klabu na atafanya hivyo katika kipindi chote cha mpito kuelekea mabadiliko ya kimuundo ya klabu,".
  Mohamed 'Mo' Dewji (kulia) akiwa na Rais wa Simba SC, Evans Aveva 

  Mbali ya hayo, Manara amesema mfanyabiashara huyo mkubwa barani Afrika atalipia kodi za nyasi bandia na gharama nyingine za uendeshaji wa klabu.
  "Uongozi wa Simba unamshukuru sana MO, ukizingatia klabu kwa sasa haina mdhamini na unaamini uwekezaji huo ni chachu ya kuwarejeshea furaha wanasimba na hatimae kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya msimu huu na misimu mingi ijayo,".
  Aidha, Manara amewaomba mashabiki wake wajitokeze kwa wingi Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishangilia timu hiyo itakapocheza na mahasimu wao wa jadi, Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  "Tunaamini mechi hiyo ni mwendelezo wa furaha kwa wanachama na washabiki wetu kote nchini. Pia tuwaombe sana kukumbuka kununua tiketi kwa mawakala wa Selcom waliopo katika maeneo mbalimbali. Ikumbukwe tiketi za mechi hii ni za kieletroniki,"amesema Manara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MO DEWJI ANAMWAGA FEDHA TU SIMBA...SASA MSIMBAZI NI BWAWA LA NEEMA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top