• HABARI MPYA

  Jumanne, Septemba 27, 2016

  REFA ALIYEFUNGIWA KWA KUVURUNDA APEWA SIMBA NA YANGA J’MOSI TAIFA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  REFA aliyewahi kufungiwa kwa kuvurunda mechi, Martin Saanya ameteuliwa kuchezesha mchezo baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Saanya mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), alifungiwa mwaka mmoja na uongozi uliopita wa TFF, chini ya Rais Leodegar Tenga kwa tuhuma za kuvurunda mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga na Coastal Union iliyomalizika kwa sare ya 1-1 msimu wa 2013/14.
  Martin Saanya ameteuliwa kuchezesha mchezo baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  Lakini, chini ya uongozi mpya wa TFF wa Rais Jamal Malinzi, Sanya akafutiwa adhabu na kuendelea na kazi – na Jumamosi atachezesha mchezo mwingine mkubwa wa Ligi Kuu baina ya watani, Simba na Yanga. 
  Mara ya mwisho Saanya kuchezesha mechi kubwa ilikuwa msimu uliopita alipopuliza kipyenga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Yanga ikiifuga Azam.
  Lakini pia hii si mara ya kwanza kwa Saanya kuchezesha mechi ya watani, kwani msimu wa 2013/2014 alichezesha mchezo ambao Yanga ilishinda 2-0 mabao ya Hamisi Kiiza na Didier kavumbangu.
  Katika mchezo huo, Saanya aliumia jicho wakati akiamulia ugomvi baina ya waliokuwa wachezaji wa timu hizo, mshambuliaji Mrundi wa Yanga, Didier Kavumbangu na beki Mzanzibari wa Simba SC, Nassor Masoud 'Chollo' na kutibiwa kwa dakika tatu. 
  Saanya akimdhibiti mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbangu (kushoto) asipigane na beki wa Simba SC, Nassor Masoud 'Chollo' (kulia) mbele ya kocha wake, Mfaransa, Patrick Liewig  

  Refa huyo akapewa tena mchezo mwingine wa watani msimu wa 2014/15, Simba ikishinda 1-0, bao pekee la Mganda Emmanuel Okwi.
  Na katika mchezo wa Jumamosi, Saanya atasaidiwa na Samwel Mpenzu na Ferdinand Chacha.
  Viingilio katika mchezo huo vinatarajiwa kuwa Sh 7,000, 10,000, 20,000 na 30,000.
  Yanga imeweka kambi kisiwani Pemba na Simba ipo Morogoro kujiandaa na mchezo huo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: REFA ALIYEFUNGIWA KWA KUVURUNDA APEWA SIMBA NA YANGA J’MOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top