• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 28, 2016

  MANJI AIPA YANGA SC ENEO LA EKARI 715 UFUKWENI KUJENGA UWANJA WA KISASA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Yanga SC, Yussuf Mehboob Manji ameipa klabu hiyo eneo la ekari 715 ufukweni mwa Bahari ya Hindi, upande wa Geza Ulole, Kigamboni, Dar es Salaam.
  Wasaidizi wa Manji wamekabidhi eneo hilo leo mchana katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na Maofisa wa chama na Serikali ya Kigamboni.
  Aliyepokea eneo hilo kwa niaba ya klabu ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu, Mama Fatma Karume aliyeambatana na Mjumbe mwingine wa Bodi hiyo, Dk. Jabir Idris Katundu, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu, Samuel Lukumay na Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit.
  Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Mama Fatma Karume (katikati kulia) akifunua jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa klabu katika eneo lililotolewa na Mwenyekiti, Yussuf Manji, Geza Ulole, Dar es Salaam
  Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchembaa akizungumza katika hafla hiyo
  Diwani wa Kigamboni, Doto Msaka (kushoto) akizungumza katika hafla hiyo
  Sehemu ya eneo la ekari 715 ambalo Manji amewapa Yanga wajenge Uwanja wa kisasa
  Wadau mbalimbali mbele ya jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa Yanga 
  Vijana wakicheza ngoma katika hafla hiyo leo Geza Ulole, Dar es Salaam

  Akizungumza katika hafla hiyo, Mama Karume, mke wa rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume alisema kwamba Baraza lake lilikuwa na kikao na Mwenyekiti wa klabu, Manji kabla ya hatua hiyo.
  “Baada ya wanachama kuomba wenyewe katika Mkutano Mkuu kwamba wanataka Uwanja, sisi tulikaa na Mwenyekiti na tukakubaliana juu ya jambo hili,”alisema.
  Kwa upande wake, Waziri Nchemba ambaye ni mpenzi na mwanachama wa Yanga, alisema kwamba alimuambia Manji aachane na ndoto za kufikiria kuuendeleza Uwanja wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu kwa sasa, Jangwani, Dar es Salaam na kutafuta eneo la lingine.      
  “Nilimuambia Manji, kuendelea kufikiria Kaunda ni kujidanganya. Wakati wenzetu (Simba) wanakwenda Bunju, sisi twende Kigamboni,”alisema Nchemba na kuongeza; “Na maana ya Geza Ulole ni Jaribu uone, tukiwa na Uwanja huku, kila atakayejaribu kuja tutamfunga,”alisema kwa utani na kumpongeza Manji kwa hatua hiyo.
  Waziri Nchemba akampongeza pia na Mama Karume kwa kuwa bega kwa bega na klabu kwa miaka mingi; “Tunajivunia unavyolibeba suala hili kwa uzito tangu ujana wako,”alisema.
  Mwigulu pia akasema zawadi ya Manji ni chachu kwa klabu kushinda mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  “Uendeshwaji wa klabu kisasa, ni jambo ambalo lilitakiwa litokee miaka iliyopita si sasa. Wakati Yanga inacheza na Al Ahly (ya Misri), Rais wa Mazembe (Moise Katumbi) alisema hii ni moja ya klabu bora Afrika.
  Sasa baada ya kuwa na Uwanja itakuwa bora zaidi,”alisema.
  Diwani wa Kigamboni, Dotto Msaka aliwakaribisha Yanga Kigamboni na akasema klabu hiyo itakuwa tishio maradufu ikianza rasmi maisha ya Geza Uloe, huku akiweka wazi kwamba na yeye pia ‘Kandambili’.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANJI AIPA YANGA SC ENEO LA EKARI 715 UFUKWENI KUJENGA UWANJA WA KISASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top