• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 22, 2016

  AZAM WAIFUATA NDANDA FC NA STAILI TOFAUTI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imeondoka leo mchana kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Ndanda FC Jumamosi Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
  Na Kocha Mkuu wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Zeben Hernandez Rodriguez, amekiweka sawa kikosi chake kukabiliana na kila hali katika mchezo huo.
  Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na lengo moja tu la kuhakikisha inaibuka na ushindi kutokana na kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Simba (1-0) licha ya kuonyesha kiwango bora kwa asilimia kubwa ya mechi hiyo.
  Rodriguez (katikati) akiwa na Wasaidizi wake katika moja ya michezo ya Ligi Kuu

  “Tutabadilisha aina yetu ya mpira kwa sababu uwanja tutakaochezea ni mbaya sana, tunauchukulia kwa uzito mkubwa sana mchezo huo, tutacheza soka la mipira mirefu sana lakini kwa urahisi, hili ni jambo la muhimu sana kutokana na aina ya uwanja tutakaochezea,” alisema.
  Ili kuonyesha amepania kukabiliana na uwanja huo pamoja na wapinzani wake, Kocha huyo raia wa Hispania kwa siku mbili hizi tokea jana hadi kesho asubuhi, amekuwa akikipika kikosi chake katika uwanja wa nyasi za kawaida unaoendana kidogo na Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
  Zeben alisema kuwa jambo la muhimu kwa leo na kesho ni baadhi ya wachezaji waliocheza mchezo uliopita kufanya mazoezi ya kurudisha miili yao vizuri kabla ya kuamua kikosi kitakachokwenda kuikabili Ndanda, kitakachosafiri kesho Alhamisi mchana.
  “Kwangu mimi mchezo uliopita (Simba) ulikuwa mzuri kwa timu yangu, tulikuwa bora mchezoni zaidi ya Simba, lakini kwa kosa moja tulilolifanya Simba waliweza kulitumia na kufunga bao, kwa sasa ninachofanya ni kuwaweka sawa wachezaji wangu na muhimu kwangu kwa sasa ni kuweka akili yetu kwa mchezo ujao na kuachana na habari za mchezo uliopita,” alisema.
  Mpaka sasa katika msimamo wa ligi hiyo hadi raundi ya tano inamalizika, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola kinachosisimua koo, inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 10 sawa na Yanga iliyo nafasi ya pili huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 13 ilizojikusanyia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM WAIFUATA NDANDA FC NA STAILI TOFAUTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top