• HABARI MPYA

    Wednesday, September 21, 2016

    TUNA SAFARI NDEFU SANA WATANZANIA KUYAELEKEA MAFANIKIO

    KUNA wakati huwa natazama Wazungu wanavyofurika kwenye viwanja vyao wakati wa mechi mbalimbali, hata zile za timu ambazo sisi tunaamini ni ndogo, halafu najiuliza kwa nini hawa watu wasifanikiwe?
    Wanapenda mchezo. Wanakwenda kwa wingi viwanjani. Wanapenda timu zao. Kila timu iliyosajiliwa Uingereza, Hispani, Italia, Ujerumani ina mashabiki wa kujaza Uwanja wake. 
    Miezi miwili iliyopita ilifanyika michuano ya Euro nchini Ufaransa na Ureno wakafanikiwa kutwaa Kombe – tulishuhudia Wazungu kutoka nchi zote zilizoshiriki mashindano hayo wakiwa wamefurika huko.
    Sasa rudi kwetu Afrika – kielelezo ni fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 Afrika Kusini ambavyo tulishindwa kuzitumia kuishawishi FIFA itupe uenyeji wa fainali nyingine japo baada ya miongo miwili.
    Huku Tanzania ndiyo kabisaa. Yaani tunajifanya tunapenda michezo, wakati ukweli ni kwamba hatuipendi michezo.
    Tanzania tunapenda Simba na Yanga tu, zaidi ya hapo hatujaonyesha mapenzi ya dhati kwenye michezo.
    Tungekuwa tunapenda michezo timu zetu huko mikoani zisingekuwa zinacheza viwanja vitupu. Tungekuwa tunapenda michezo hata Mungu angesikia kilio chetu cha mafanikio.
    Lakini kama hatupendi michezo, hayo mafanikio yatatustahili vipi?
    Jana timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania, Kilimanjaro Queens imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kuwafunga Kenya mabao 2-1 Uwanja wa Ufundi, Jinja.
    Shukraani kwao, wafungaji wa mabao hayo, Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’ na Stumai Abdallah dhidi ya moja la Kenya, lililofungwa na Christine Nafula.
    Awali, Tanzania Bara iliongoza Kundi B baada ya kushinda kura ya sarafu kufuatia sare ya 0-0 na Ethiopia katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo, hivyo kufungana nayo kwa pointi na wasatani wa mabao kileleni. 
    Kilimanjaro Queens ilianza vizuri michuano hiyo kwa kuibamiza 3-2 Rwanda, mabao yake yakifungwa na Asha Rashid ‘Mwalala’ dakika za 11 na 65 na Stumai Abdallah dakika ya 28, wakati ya wapinzani wao yalifungwa na Ibangarrue Marie na Amina Ally wa Tanzania Bara aliyejifunga.
    Baada ya ushindi wa jana, mapema Alfajiri ya leo Kilimanjaro Queens wamepanda basi Jinja kurejea nyumbani Tanzania wakipitia Bukoba baada ya kazi nzuri waliyoifanya katika wiki zao mbili za kuwa Uganda.
    Ikumbukwe Queens waliondoka pia kwa basi kwenda Uganda kushiriki mashindano hayo, wakipitia Bukoba pia ambako walicheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Burundi na kushinda 1-0.
    Ushindi wa Kombe la kwanza la kwanza la wanawake la Challenge ni heshima kubwa kwetu kisoka – lakini ajabu haujawa na mashiko yoyote.
    Naamini, ushindi kama huu wangeupata wanaume hata katika mashindano ya nyumbani ungekuwa na mashiko makubwa na tungesikia ngonjera nyingi za wapenda sifa wa nchi hii.
    Najaribu kujiuliza, mwanamke wa Tanzania ni mnyonge kiasi gani hadi timu ya taifa inarejea kwa basi baada ya kazi nzuri waliyoifanya. 
    Mwaka 1993, Yanga SC walikwenda Uganda kwa meli ya mizigo kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame.
    Wakafanikiwa kutwaa Kombe na hawakurudi tena na meli, walitumiwa ndege na Serikali na wakapokewa kifalme pale Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal One).
    Najiuliza iwapo ni Rwanda ndiyo wangetwaa Kombe la CECAFA Challenge la wanawake, Rais Paul Kagame angewafanyia nini wachezaji wake. Wangesafiri kwa basi kurejea Kigali hata kama walikwenda kwa basi?
    Sisi timu yetu imetwaa Kombe, inarejea nalo kwa basi – sasa sijui mapokezi yatakuwa Ubungo, Kibaha au Chalinze! Tuna safari ndefu sana Watanzania kupata kile tunacholilia. Mafanikio. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNA SAFARI NDEFU SANA WATANZANIA KUYAELEKEA MAFANIKIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top