• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 26, 2016

  YANGA WAENDA PEMBA KUFUFUA MAKALI WAUE MNYAMA OKTOBA 1

  Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
  MABINGWA watetezi, Yanga SC wameondoka leo asubuhi Mwanza kwa ndege kuelekea Pemba kwa kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu, Simba SC Oktoba 1, mwaka huu.
  Yanga iliondoka Shinyanga Alfajiri ya leo baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana kwa kufungwa 1-0 na wenyeji Stand United, Uwanja wa Kambarage, bao pekee Athanas Pastory.
  Yanga SC wamekwenda Pemba kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam 

  Yanga inayobaki na pointi zake 10 baada ya mechi sita, itahitaji ushindi Oktoba 1 kujiweka sawa kwenye mbio za ubingwa.
  Kocha Hans van der Pluijm alionyesha hasira zake wazi baada ya kipigo cha jana akiwafokea baadhi ya wachezaji kwa makosa yao ya uwanjani.
  Hiyo inamaanisha kambi ya wiki moja Pemba itakuwa chungu kwa baadhi ya wachezaji kwa sababu kocha huyo Mholanzi anajua umuhimu wa kushinda mechi dhidi ya Simba, hususan wakitoka kupoteza mechi.
  Ikumbukwe Simba SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 16 za mechi sita, wakishinda tano na sare moja, wakati Stand sasa ni ya pili kwa pointi zake 12, Ndanda FC wa tatu kwa pointi zake 11. 
  Msimu uliopita, Pluijm aliiongoza Yanga kushinda mechi zote dhidi ya Simba, 2-0 kila mechi, lakini msimu huu chini ya kocha mpya Mcameroon, Joseph Marius Omog, Wekundu wa Msimbazi wanaonekana kuimarika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAENDA PEMBA KUFUFUA MAKALI WAUE MNYAMA OKTOBA 1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top