• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 30, 2016

  SAMATTA AIBUKA KIPINDI CHA PILI GENK YAUA 3-1 EUROPA LEAGUE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ametokea benchi timu yake, KRC Genk ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Sassuolo ya Italia Uwanja wa Laminus Arena, Genk katika mchezo wa Kundi F Europa League.
  Samatta aliyekosa mechi mbili zilizopita kwa kuwa majeruhi, leo aliingia dakika ya 75 kuchukua nafasi ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis wakati huo tayari Genk inaongoza 3-1.
  Mabao ya Genk leo yamefungwa na washambuliaji Karelis dakika ya nane, Mjamaica Leon Bailey dakika ya 25 na kiungo Mbelgiji Thomas Buffel dakika ya 61, wakati bao pekee la wageni lilifungwa na Matteo Politano dakika ya 65.
  Samatta ametokea benchi KRC Genk ikishinda 3-1 dhidi ya Sassuolo ya Italia katika Europa League

  Samatta hakuwepo wakati Genk inafungwa 2-0 katika Ligi ya Ubelgiji Septemba 18 na Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena na nyingine Kombe la Ligi ya Ubelgiji, wakishinda 4-0 Septemba 21 ugenini dhidi ya Eendracht Aalst Uwanja wa Het Pierre Cornelisstadion, Aalst.

  Lakini baada ya kupata ahueni, leo kocha Mbelgiji Peter Maes amempa dakika 15 za mwisho kuelekea mchezo wa Jumapili dhidi ya Mechelen katika Ligi Kuu ya Ubelgiji Uwanja wa Laminus.
  Samatta aliumia katika mchezo wa kwanza wa Kundi F Europa League dhidi ya Rapid Viena Septemba 15 Uwanja wa Allianz, Viena, Austria, KRG Genk ikifungwa 3-2.
  Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 26 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na nane msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
  Katika mechi hizo, ni 14 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na nne msimu huu – na mechi tisa hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na tatu msimu huu.
  Kikosi cha KRC Genk leo kilikuwa: Bizot, Walsh, Brabec, Colley, Nastic, Ndidi, Pozuelo, Susic/Kumordzi dk81, Buffalo/Trossard dk85, Bailey na Karelis/Samatta dk75.
  Sassuolo Calcio: Consigli, Magnanelli, Pellegrini/Mazzitelli dk65, Biondini/Ragusa dk57, Defrel, Peluso, Acerbi, Politano, Lirola, Ricci/Caputo dk79 na Letschert.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AIBUKA KIPINDI CHA PILI GENK YAUA 3-1 EUROPA LEAGUE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top