• HABARI MPYA

  Jumanne, Septemba 27, 2016

  YANGA WAMKATIA RUFAA MCHEZAJI WA STAND UNITED

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imewasilisha barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga klabu ya Stand United kumtumia mchezaji Frank Khamis Igobela katika mchezo wa Jumapili.
  Yanga ilifungwa 1-0 na Stand United Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na baada ya mchezo ikawasilisha rufaa.
  Yanga inadai Stand United imemtumia Igobela kimakosa kwa kuwa bado ni mchezaji halali wa Polisi ya Zanzibar.
  Chanzo cha habari kutoka Yanga SC kimesema kwamba, klabu imepata taarifa za kutosha kutoka Polisi ya Zanzibar juu ya mchezaji huyo.
  Makocha wa Yanga, Juma Mwambusi (kulia) na Hans van der Pluijm (kushoto) 
  Na Yanga wanadai kwamba wana ushahidi hadi wa barua ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kikiizuia TFF kumuidhinisha mchezaji huyo kucheza Ligi Kuu hadi amalizane na Polisi.
  Na Yanga wanadai wanaamini Igobela alicheza mechi ya Jumapili akiwa hana leseni, lakini wamejaribu kufuatilia TFF tangu jana hawajapata majibu.
  Yanga iliondoka Shinyanga Alfajiri ya jana kwenda Mwanza kuunganisha ndege ya kuwapeleka Dar es Salaam, baadaye Pemba kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo ujao, dhidi ya mahasimu, Simba SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na wakati ikiendelea na maandalizi ya mchezo huo wa Jumamosi, Yanga inayofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm inapigania ushindi wa mezani baada ya kipigo cha Stand kilichotokana na bao pekee la Athanas Pastory.
  Yanga inayobaki na pointi zake 10 baada ya mechi sita, itahitaji ushindi Oktoba 1 kujiweka sawa kwenye mbio za ubingwa na kocha Pluijm alionyesha hasira zake wazi baada ya kipigo cha Jumamosi akiwafokea baadhi ya wachezaji kwa makosa yao ya uwanjani.
  Hiyo inamaanisha kambi ya wiki moja Pemba itakuwa chungu kwa baadhi ya wachezaji kwa sababu kocha huyo Mholanzi anajua umuhimu wa kushinda mechi dhidi ya Simba, hususan wakitoka kupoteza mechi.
  Ikumbukwe Simba SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 16 za mechi sita, wakishinda tano na sare moja, wakati Stand sasa ni ya pili kwa pointi zake 12, Ndanda FC wa tatu kwa pointi zake 11. 
  Msimu uliopita, Pluijm aliiongoza Yanga kushinda mechi zote dhidi ya Simba, 2-0 kila mechi, lakini msimu huu chini ya kocha mpya Mcameroon, Joseph Marius Omog, Wekundu wa Msimbazi wanaonekana kuimarika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAMKATIA RUFAA MCHEZAJI WA STAND UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top