• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 30, 2016

  YANGA HATA IWE BORA, KUIFUNGA SIMBA KWA MBINDE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  UKIONDOA ushindi wa 5-0 Juni 1 mwaka 1968, ushindi mwingine mkubwa wa Yanga dhidi ya Simba umekuwa ni 3-0.
  Na ushindi huo waliupata kwenye mchezo wa kirafiki, Aprili 20, mwaka 2003 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mabao ya Kudra Omary dakika ya 30, Heri Morris dakika ya 32 na Salum Athumani dakika ya 47.
  Zaidi ya hapo, sana Yanga imekuwa ikiifunga Simba 3-1, au 2-0. 
  Maajabu yalikaribia kutokea Oktoba 20, mwaka 2013, Yanga ilipomaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza inaongoza 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini kipindi cha pili, Simba wakasawazisha mechi ikaisha 3-3.
  Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto akimtoka kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko
  Mabao ya Yanga iliyokuwa chini ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts yalifungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 15 na Hamisi Kiiza mawili dakika ya 36 na 45, wakati ya Simba iliyokuwa chini ya Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ yalifungwa na Betram Mombeki dakika ya 54, Joseph Owino dakika ya 58 na Gilbert Kaze dakikaa ya 85.
  Katika historia ya mechi za watani wa jadi kwenye soka ya Tanzania, Yanga wanajivunia kushinda mechi nyingi, wakati Simba wanatambia kushinda mabao mengi katika mchezo mmoja, 6-0.
  Lakini Yanga wanaamini walifungwa na Simba 6-0 kwa sababu walikuwa wametoka kwenye mgogoro mkubwa mwaka 1976 ulioigawa klabu yao hadi kuzaliwa Pan African.
  Baada ya mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni, rasilimali nyingi za klabu hiyo, yakiwemo mabasi ziliteketea. Lakini pengine hilo inawezekana lisiwaumize sana wana Yanga, kuliko kipigo kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba, cha mabao 6-0.
  Baada ya mgogoro huo, kwa sababu wachezaji wote walimfuata mzee Tarbu Mangara aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yanga walilazimika kuunda upya timu yao, wakisajili wachezaji wapya. Tangu mwaka 1977, Yanga walikuwa vibonde wa Simba hadi mwaka 1981, walipojikomboa.
  Tangu kuanzishwa kwa Ligi ya Tanzania, mwaka 1965 hadi mwaka 1976 Yanga inakutwa na mgogoro huo, ilikuwa imekutana na watani wao wa jadi, Simba kwenye mechi 10. Katika mechi hizo, Yanga walishinda saba, Simba waliibuka kidedea mara mbili na mara moja ilikuwa ni sare.  
  Kati ya mara saba ambazo Yanga iliifunga Simba, ndani yake kuna kipigo cha mabao 5-0, Juni Mosi mwaka 1968, enzi hizo Simba bado ikiitwa Sunderland. 
  Siku hiyo, mabao ya Yanga yalitiwa kimiani na Maulid Dilunga dakika za 18 kwa penalti na 43, wakati mengine yalifungwa na Salehe Zimbwe dakika za 54 na 89 na kuhitimisha karamu ya mabao, lilifungwa na Kitwana Manara 'Popat' dakika ya 86.
  Kwa homa ya kipigo hicho, kwenye mchezo uliofuata Machi 3, mwaka 1969, Simba waliishia njiani maeneo ya Chang'ombe na kurejea klabuni kwao, wakihofia kutandikwa zaidi, hivyo watani wao wa jadi, kupewa pointi za chee.
  Baada ya hapo, timu hazikukutana hadi Juni 4, mwaka 1972, Simba wakiwa madhubuti tayari kuweza kuhimili vishindo vya Yanga. Katika mchezo huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, tena Sunderland ikitangulia kupata bao kupitia mshambuliaji wake, Willy Mwaijibe, dakika ya 11, kabla ya Kitwana Manara kusawazisha dakika nane baadaye.
  Juni 18, mwaka huo huo 1972, timu hizo zilikutana tena na bao pekee la Leonard Chitete (sasa marehemu) lilitosha kuendeleza ubabe wa Yanga kwa Simba.
  Haidari Abeid 'Muchacho' alikomesha tabia ya Simba kufungwafungwa na Yanga, katika mechi baina ya watani hao wa jadi, Juni 23, mwaka 1973, akifunga bao pekee lililowalaza mapema wana Jangwani, dakika ya 68. 
  Wakati Simba ikiamini imekwishapata dawa ya Yanga, Agosti 10, mwaka 1974 katika mchezo uliowakutanisha watani hao wa jadi nje ya Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza, Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Wekundu wa Msimbazi walikiona cha moto.
  Wekundu wa Msimbazi walianza vizuri kwa kuwatungua Yanga bao la mapema dakika ya 16 tu ya mchezo, mfungaji akiwa ni Adamu Sabu. Lakini zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika, mjini Dar es Salaam, mashabiki wa Simba wakiwa wamekwishajikusanya kuanza misafara ya kuelekea makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Msimbazi kushangilia ushindi, walikuwa wanyonge ghafla baada ya mtangazaji wa Radio Tanzania (RTD), Ahmad Jongo kutangaza bao la kusawazisha la Gibson Sembuli (sasa marehemu).
  Kwa bao hilo, mchezo huo kwa sababu ulikuwa wa kuamua bingwa, ilibidi uhamie kwenye dakika 30 za nyongeza. Dakika ya saba Sunday Manara aliwainua vitini mashabiki wa Yanga waliokuwa Nyamagana kwa kufunga bao la pili. Naam, huo ulikuwa ushindi wa mwisho wa Yanga kwa Simba, kwani baada ya hapo, mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna klabu hiyo.
  Hatimaye ikawadia siku chungu zaidi katika maisha ya Yanga kwenye utani wao na Simba, ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, enzi hizo Simba ikinolewa na Mbulgaria, Dimitar Samsarov.
  Simba ikiwa na 'mziki' wake ule ule uliokuwa ukichuana na Yanga tangu mwaka 1974, ilikutana na Yanga mpya kabisa iliyoundwa na wachezaji kama kipa aliyekuwa Mwadui ya Shinyanga, Bernard Madale.
  Yanga walishindwa kuimudu kasi ya Simba na kujikuta wakitandikwa mabao 6-0, mabao ya Wekundu wa Msimbazi yakitiwa kimiani na Abdallah Kibadeni katika dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73, wakati Selemani Sanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20. Kipigo hicho kilikuwa sababu tosha ya kipa Madale kutupiwa virago Jangwani. 
  Lakini Yanga iliendelea kuchezea vipigo tu walipokutana na Simba, japokuwa Oktoba 7, mwaka 1979 walipunguziwa dozi kwa kiwango cha nusu nzima, kutoka bao sita hadi tatu. 
  Yanga ilichapwa 3-1 siku hiyo, mabao ya Simba yakifungwa na Nico Njohole dakika ya tatu, Mohammed Bakari 'Tall' dakika ya 38 na Abbas Dilunga dakika ya 72, wakati lile la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Rashidi Hanzuruni dakika ya nne.
  Oktoba 4, mwaka 1980, Yanga ilipigwa tena 'nusu dozi' ya 6-0, mabao ya wana Msimbazi yakitiwa kimiani na Abdallah Mwinyimkuu dakika ya 29, Thuwein Ally dakika ya 82 na Nico Njohole dakika ya 83.
  Hatimaye saa ya ukombozi iliwadia Jangwani, Juma Hassan Mkambi akiitwa 'Jenerali' enzi zake alikomesha uteja wa Yanga kwa Simba, Septemba 5, mwaka 1981, kwa bao lake pekee dakika ya 42. Siku hiyo, mabeki wa Yanga walifanya kazi kubwa ya kulinda bao hadi dakika 90 zilipotimia, wana Jangwani wanainua mwali wao.
  Naam, Mkambi alifuta uteja wa Yanga kwa Simba na kuanzisha rasmi enzi za Jangwani kuwanyima raha wana Msimbazi, kwani katika mechi iliyofuata, Aprili 29, mwaka 1982, bao la Rashid Hanzuruni dakika ya pili tu ya mchezo liliifanya Simba ilale tena 1-0.
  Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kuwakutanisha watani wa jadi, tangu kuanza kwa Ligi ya Bara kutoka Klabu Bingwa ya Taifa na katika mchezo wa marudiano, Simba walikiona tena cha moto, walitandikwa 3-0, Septemba 18, mwaka huo, 1982.
  Mabao ya Yanga siku hiyo yalitiwa kimiani na Omar Hussein 'Keegan'
  katika dakika ya pili na ya 85, wakati lingine lilifungwa na Makumbi Juma 'Homa ya Jiji' au 'Bonga Bonga' dakika ya 62.
  Tangu hapo, Yanga iliitesa Simba kwa miaka sita mfululizo, hadi ilipokuja kujikomboa Agosti 23, mwaka 1986 kwa ushindi wa mabao 2-1, wafungaji wakiwa ni marehemu Edward Chumila, dakika ya tisa na Malota Soma dakika ya 51. Siku hiyo Omar Hussein alitangulia kuifungia Yanga bao dakika ya 5.
  Februari 10, mwaka 1983, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa marudiano, Aprili 16, mwaka huo, Yanga ilishinda 3-1, mabao yake yakitiwa kimiani na Charles Boniface Mkwasa dakika ya 21, Makumbi Juma dakika ya 38 na Omar Hussein dakika ya 84, wakati la kufutia machozi la Simba lilifungwa na marehemu 'Super' Kihwelo Mussa dakika ya 14.
  Septemba 10, mwaka 1983, Yanga iliichapa Simba 2-0, wafungaji wakiwa ni Lila Shomari aliyejifunga dakika ya 72, kabla ya Ahmad Amasha kufunga la pili dakika ya 89, wakati kwenye mechi ya marudiano, Septemba 25, mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1. Sunday Juma 'Pikipiki' alitangulia kuifungia Simba bao dakika ya 72, kabla ya Makumbi Juma kusawazisha dakika tatu baadaye, dakika ya 75.
  Machi 10, mwaka 1984, timu hizo zilitoka 1-1 tena, kipa Iddi Pazi 'Father' akitangulia kuifungia Simba bao kwa mkwaju wa penalti dakika ya 20, kabla ya Omar Hussein kusawazisha dakika ya 72.
  Julai 14, mwaka 1984, mdudu wa sare aliendelea kutawala kwa watani wa jadi, kwani zilitoka 1-1 tena, Zamoyoni Mogella 'Golden Boy' akitangulia kuifungia Simba dakika ya 17, kabla ya Abeid Mziba 'Tekero' kusawazisha dakika ya 39.
  Mei 19, mwaka 1985 mchezo ulimalizika kwa sare ya 1-1 tena, Omar Hussein akianza kuifungia Yanga dakika ya sita kabla ya Mohammed Bob Chopa kuisawazishia Simba dakika ya 30.
  Yanga ilirejesha enzi za ubabe Agosti 10, mwaka 1985, ilipopewa pointi za chee, baada ya Simba kutoroka uwanjani ikigomea adhabu ya penalti, wakati Machi 15, mwaka 1986 zilitoka sare ya 1-1 tena, John Hassan Douglas akitangulia kuifungia Simba dakika ya 20, kabla ya Abeid Mziba kusawazisha dakika ya 44.
  Katika mchezo wa marudiano, Agosti 23, 1986 ndiyo Chumila na Malota walizima ubabe wa Yanga kwa Simba rasmi.
  Baada ya hapo, timu hizo zilikuwa zikifungana kwa zamu, ingawa kipigo kikali zaidi kilikwenda kwa Yanga, Julai 2, mwaka 1994, wakati Simba waliposhinda 4-1.
  Hata hivyo, baada ya mchezo huo, Yanga ilivunja tena kikosi kutokana na tuhuma za kuhujumiwa na wachezaji wake, safari hiyo ikidaiwa aliyekuwa mfadhili mmoja wa klabu hiyo mwenye asili ya Kiasia, aliwapa fedha wachezaji wafungwe ili kuwakomoa viongozi katika vita iliyokuwa inaendelea baina yao.
  Baadhi ya wachezaji waliobakishwa kikosini walikuwa ni Kenneth Mkapa, Constantine Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, wengine wote walitimuliwa kwa tuhuma hizo.
  Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) katika kikosi cha pili, ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh, Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan African.
  Baada ya hapo, Simba ilirejesha utemi wake kwa Yanga kwa kuifunga mfululizo tangu mwaka 2004 hadi ilipojikomboa Oktoba 26, mwaka 2008, kwa bao pekee la Ben Mwalala dakika ya 15 ya mchezo huo, Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam.
  Yanga ilikuwa imeifunga Simba kwa mara ya mwisho katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Aprili 20, mwaka 2003, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao 3-0 yaliyotiwa kimiani na Heri Morris, Salum Athumani na Kudra Omar.
  Katika Ligi Kuu, Yanga ilikuwa imeifunga Simba kwa mara ya mwisho Agosti 5, mwaka 2000, mabao 2-0 yote yakifungwa na Iddi Moshi Shaaban, anayechezea Villa Squad kwa sasa.
  Moshi, aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza tangu ametoka kwenye fungate la ndoa yake, alifunga mabao hayo katika dakika za 37 na 47, wakati kwenye mechi iliyofuata Septemba 1, mwaka 2001, bao pekee la Joseph Kaniki 'Golota' katika dakika ya 76 liliinyima raha Yanga siku hiyo.
  Sekilojo Chambua, ambaye kwa sasa ni kocha, aliinusuru Yanga kulala tena mbele ya Simba Septemba 30, mwaka 2001, baada ya kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 86, kufuatia Kaniki tena kutangulia kufunga dakika ya 65 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. 
  Agosti 18, mwaka 2002, Chambua tena aliinusuru Yanga kulala, baada ya mwamuzi Victor Mwandike kuipa timu hiyo penalti dakika ya 89 na kiungo huyo wa zamani kuukwamisha mpira kimiani.
  Awali ya hapo, mkongwe Madaraka Suleiman 'Mzee wa Kiminyio', alitangulia kuifungia Simba bao dakika ya 65, wakati mechi ya marudiano Novemba 10, mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
  Septemba 28, mwaka 2003, mabao ya Kudra Omary dakika ya 42 na Heri Morris dakika ya 55, yaliinusuru Yanga kulala 2-0 mbele ya Simba, kufuatia Emanuel Gabriel kufunga mapema katika dakika za 27 na 36, wakati kwenye mchezo wa marudiano Novemba 2, mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
  Agosti 7, mwaka 2004, Shaaban Kisiga alitangulia kuifungia Simba dakika ya 64, kabla ya Pitchou Kongo kusawazisha dakika tatu tangu kuanza kipindi cha pili na Ulimboka Mwakingwe kufunga bao la ushindi dakika ya 76.
  Bao pekee la Athumani Machuppa katika dakika ya 82, liliipa ushindi wa 1-0 Simba dhidi ya Yanga Septemba 18, mwaka 2004, wakati Aprili 17, mwaka 2005 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Aaron Mwinura Nyanda alitangulia kuifungia Yanga dakika ya 39, kabla ya Nurdin Msiga kuisawazishia Simba dakika ya 44 na Machuppa kufunga la pili dakika ya 64.
  Kwenye mchezo wa marudiano, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha uliofanyika Agosti 21, mwaka 2005, Nicodemus Nyagawa aliibuka nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao yote mawili yaliyoipa Simba ushindi wa 2-0 dhidi ya Yanga, dakika za 22 na 56.
  Machi 26, mwaka 2006, baada ya Yanga kuimarisha kidogo kikosi chake, ilianza kugoma kufungwa kwa kulazimisha sare ya bila kufungana na Simba kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa marudiano Oktoba 29, mwaka huo, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Julai 8, mwaka 2007 katika fainali ya Ligi ndogo ya Bara, Moses Odhiambo alitangulia kuifungia Simba kwa mkwaju wa penalti dakika ya pili tu ya mchezo, kabla ya Said Maulid 'SMG' kufunga la kusawazisha dakika ya 55.
  Mchezo huo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare hiyo.
  Oktoba 24 mwaka 2008, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Simba wakicheza 10 baada ya Henry Joseph kutolewa kwa kadi nyekundu mapema tu dakika ya sita, iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Ulimboka Mwakingwe dakika ya 23.
  Aprili 27 mwaka 2009 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu, timu zilitoka sare ya bila kufungana na Oktoba 26, mwaka 2008, Ben Mwalala alifunga bao dakika ya 15, ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo, hivyo kuifutia Yanga uteja uliodumu tangu mwaka 2004.
  Bao la Mwalala lilikuwa la kishujaa na la kihistoria kama ilivyokuwa kwa Jenerali Mkambi, Septemba 5, mwaka 1981.
  Katika mchezo wa marudiano kwenye Ligi hiyo, baina ya watani hao wa jadi, Aprili 19, mwaka 2009 Yanga ilinusurika kulala 2-1, kama si bao la Jerry Tegete dakika ya 90.
  Ramadhan Chombo 'Redondo' alitangulia kuifungia Simba kwa kichwa dakika ya 23, kabla ya Mwalala kusawazisha dakika ya 48 kwa shuti lililowababatiza mabeki na kutinga nyavuni. Haruna Moshi 'Boban' aliifungia Simba bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 62, kabla ya Tegete kuzima shangwe za wana Msimbazi, tena ndani ya dakika za lala salama.
  Oktoba 31, mwaka 2009, bao pekee la Mussa Hassa Mgosi katika dakika ya 26, lilitosha kuipa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga, Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Aprili 18, mwaka 2010 ilikuwa funga nikufunge kabla ya Weikundu wa Msimbazi kutoka kifua mbele kwa ushindi wa 4-3.
  Mabao ya Simba yalifungwa na Uhuru Suleiman dakika ya tatu, Mgosi dakika ya 53 na 74 na Mkenya Hillary Echesa dakika ya 90 na ushehe, wakati wa Yanga yaolifungwa na Athumani Iddi dakika ya 30 na Jerry Tegete dakika za 69 na 89.
  Baada ya mechi hiyo, kipa Mzungu wa Yanga, Obren Curkovic kutoka Serbia aliondoka moja kwa moja kwenye klabu hiyo, kwa aibu ya kufungwa mabao mengi na ya kuzembe, hasa la nne lililotiwa kimiani na Mkenya Echesa kwa umbali wa zaidi ya mita 40.
  Msimu uliofuata katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu mjini Mwanza, Yanga ililipa kisasi Oktoba 16, mwaka 2010 kwa bao la Jerry Tegete dakika ya 70. Ikumbukwe mapema katika kuuzindua msimu huo, Simba na Yanga zilikutana katika mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 18, mwaka 2010 na dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana.
  Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na Yanga ikashinda kwa penalti 3-1. Geoffrey Bonny, Stefano Mwasyika na Isaac Bokaye walimtungua kipa wa Simba siku hiyo, Ally Mustafa ‘Barthez’ wakati Mghana Ernest Boakye alikosa. Mohamed Banka ndiye mchezaji pekee wa Simba aliyemtungua kipa wa Yanga, Mghana Yaw Berko siku hiyo, wakati Emanuel Okwi, Uhuru Suleiman na Juma Nyosso walipoteza penalti zao.
  Wababe hao katika soka ya Tanzania, walikutana tena katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Machi 5, mwaka 2010 na dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Yanga wakitangulia kupata bao dakika ya 59 kwa penalti mfungaji Stefano Asangalwisye Mwasyika.
  Penalti hiyo ilitolewa baada ya mchezaji wa Kizambia wa Yanga, Davies Robby Mwape kuangushwa kwenye eneo la hatari na Juma Said Nyosso na refa Orden Mbaga akaamuru pigo hilo, ingawa watu walistaajabu kwa nini hakutoa kadi nyekundu kwa beki wa Simba.
  Mussa Hassan Mgosi Mgunya aliisawazishia Simba dakika ya 73, akiuwahi mpira uliotemwa na Yaw Berko, kufuatia shuti la mpira wa adhabu kutoka nje kidogo ya eneo la mita 18 lililopigwa na Mganda Emmanuel Okwi.
  Refa Orden Mbaga alizua tafrani uwanjani, kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya kujadiliana na msaidia wake namba moja.
  Oktoba 29, mwaka 2011, mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Yanga ilishinda 1-0 bao pekee la Mzambia Mwape na marudiano, Simba wakashinda 5-0 
  Mei 6, mwaka 2012 mabao Emmanuel Okwi dakika ya pili na 62, Felix Sunzu kwa penalti dakika ya 56, Juma Kaseja kwa penalti pia dakika ya 67 na Patrick Mafisango kwa penalti dakika ya 72.
  Oktoba 3, mwaka 2013 timu hizo zikatoka sare ya 1-1, Simba SC wakitangulia kwa bao la Amri Kiemba dakika ya tatu, kabla ya Said Bahanuzi kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 65.
  Mei 18, mwaka 2013, Yanga ikashinda 2-0 mabao ya Mrundi Didier Kavumbangu dakika ya tano na Mganda Hamisi Kiiza dakika ya 62.
  Hii ndiyo mechi ambayo ilimaliza historia ya kipa Juma Kasema ndani ya Simba, kwani baada ya mchezo alifukuzwa akituhuiwa kufungwa kwa urahisi bao la Kavumbangu. 
  Oktoba 20, mwaka 2013 timu hizo zilitoka sare 3-3 baada ya Yanga kuongoza kwa 3-0 hadi mapumziko, mabao ya Ngassa na Kiiza mawikli, kabla ya Simba kusawazisha kipindi cha pili kwa mabao ya Mombeki, Owino na Kaze.
  Aprili 19, mwaka 2014 zikatoka sare ya 1-1, Simba wakitangulia kwa bao la Haroun Chanongo dakika ya 76 kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga SC dakika ya 86.
  Oktoba 18, mwaka 2014 zilitoka sare ya 0-0, kabla ya Simba kushinda 1-0 Machi 8, mwaka 2015, bao pekee la Okwi dakika ya 52.
  Msimu uliopita Yanga ilishinda mechi zote 2-0 kila moja; Septemba 26, mwaka 2015 mabao ya Amissi Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79 na Februari 20, mwaka 2016 mabao ya Donald Ngoma dakika ya  39 na Tambwe dakika ya 72.
  Wanaume hao wanakutana tena Jumamosi ya kesho Uwanja wa Taifa, katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, je, nani atamlaza mwenzake mapema? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA HATA IWE BORA, KUIFUNGA SIMBA KWA MBINDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top