• HABARI MPYA

  Jumamosi, Septemba 24, 2016

  SIMBA YATUMA SALAMU YANGA, YAITANDIKA MAJI MAJI 4-0 TAIFA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imezidi kutanua kwapa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Maji Maji ya Songea jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Ushindi huo uliotokana na mabao ya Jamal Simba Mnyate mawili na moja la Shizza Ramadhani Kichuya, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 16, baada ya kucheza mechi sita, wakishinda tano na sare moja. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Ludovic Charles wa Tabora aliyesaidiwa na Anord Bugando wa Singida na Joseph Masija wa Mwanza, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Jamal Mnyate (kulia) akishangilia na Ibrahim Hajib baada ya kufunga bao la kwanza
  Mnyate akichomoka kukimbia baada ya kufunga dhidi ya Maji Maji leo
  Ibrahim Hajib akimtoka beki mkongwe wa Maji Maji, Lulanga Mapunda
  Shizza Kichuya akiwatoka mabeki wa Maji Maji leo Uwanja wa Taifa
  Beki wa Simba SC, Mohammed Hussein 'Tshabalala' akiwatoka wachezaji wa Maji Maji

  Bao hilo lilifungwa na kiungo mpya, Jamal SImba Mnyate aliyesajiliwa kutoka Mwadui FC ya Shinyanga dakika ya nne akimalizia mpira uliotemwa na kipa Aman Simba baada ya shuti la Ibrahm Hajib aliyeunganisha krosi ya Laudit Mavugo.
  Simba ikapata pigo dakika ya 21 baada ya mshambuliaji wake tegemeo, Ibrahm Hajib kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na kiungo Said Ndemla.
  Shizza Ramadhani Kichuya akaifungia Simba SC bao la pili kwa penalti dakika ya 67 baada ya beki wa Maji Maji, Lulanga Mapunda kuunawa mpira kwenye boksi.
  Mnyate akawainua tena wapenzi wa SImba vitini kwa kufunga bao la tatu dakika ya 74 akimalizia krosi ya Mo Ibrahim
  Kichuya akakamilisha sherehe za mabao za Simba SC kwa kufunga la nne dakika ya 81 baada ya kumlamba chenga kipa mkongwe wa Maji maji, Amani Simba baada ya pasi ndefu ya Nahodha Jonas Gerald Mkude.  
  Baada ya ushindi huo, Simba inakwenda kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC Jumamosi wiki ijayo Uwanja huo huo wa Taifa.  
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Janvier Besala Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk51, Laudit Mavugo/Ame Ali dk62, Ibrahim Hajib/Said Ndemla dk21 na Jamal Mnyate.  
  Maji Maji; Amani Simba, Suleiman Kibuta/Tarik Simba dk80, Bahati Yussuf, Hamad Kibopile, Ernest Raphael, Lulanga Mapunda, Alex Kondo, Luka Kikoti/Marcel Boniventura dk59, Darlington Enyina, George Mpole na Paul Maona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA YATUMA SALAMU YANGA, YAITANDIKA MAJI MAJI 4-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top