• HABARI MPYA

  Alhamisi, Septemba 29, 2016

  MANJI AMEWAPA YANGA ENEO AMBALO LINAMILIKIWA NA WATU WENGINE PIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  ENEO la ukubwa wa ekari 715 liliopo ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Geza Ulole, Kigamboni, Dar es Salaam ambalo klabu ya Yanga ilipewa na Mwenyekiti wake, Yussuf Mehboob Manji jana, lina mgogoro wa umiliki.
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata zinasema kwamba, mbali na Manji, wamiliki wengine wa eneo hilo ni pamoja na kampuni ya Lake Oil Limited.
  Na wote wanadai kuuziwa eneo hilo na Shirika la Taifa la Kilimo na Chakula (NAFCO).
  Jitihada za kuwapata mapema NAFCO kuzungumzia mgogoro huo zinaendelea – lakini taarifa za awali zinasema Manji ndiye mmiliki halali, bali wengine walivamia.
  Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Mehboob Manji jana ameipa klabu eneo lenye mgogoro wa umiliki 

  “Tatizo Manji baada ya kuuziwa eneo lile, aliliacha kwa muda mrefu bila kuliendeleza, ndipo watu wengine wakavamia, lakini mtu anayefahamika kuuziwa eneo hilo na NAFCO ni Manji,”kimesema chanzo.
  Wasaidizi wa Manji jana walikabidhi eneo hilo kwa Yanga katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.
  Aliyepokea eneo hilo kwa niaba ya klabu ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu, Mama Fatma Karume aliyeambatana na Mjumbe mwingine wa Bodi hiyo, Dk. Jabir Idris Katundu, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu, Samuel Lukumay na Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit.
  Na jiwe la msingi linaonyesha kwamba Yanga katika eneo hilo itajenga Uwanja wa kisasa na kituo cha kuendeleza vipaji vya vijana, ujenzi ambao utaanza Oktoba 28, mwaka huu.
  Juhudi za kumpata Manji kwa upande wake kuzungumzia sakata hilo zinaendelea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANJI AMEWAPA YANGA ENEO AMBALO LINAMILIKIWA NA WATU WENGINE PIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top