• HABARI MPYA

  Ijumaa, Septemba 23, 2016

  CHIRWA: NIKIPANGWA OKTOBA 1, SIMBA TUTAHESHIMIANA

  Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
  KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa Chola amesema kwamba iwapo atapangwa katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba Oktoba 1, mwaka huu atajenga heshima.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo, Chirwa amesema kwamba amekuwa akijifua kwa bidii ili kumshawishi kocha Hans can der Pluijm ampe nafasi Oktoba 1.
  “Najua bado sijawafurahisha mashabiki wa timu yangu (Yanga). Na ninajua nina deni. Lakini nawaomba watulie, mimi ninalifanyia kazi hilo,”amesema Chirwa aliyesajiliwa Julai mwaka huu kutoka Platinum FC ya Zimbabwe.
  Chirwa akiwatoka wachezaji wa Medeama SC ya Ghana katika Kombe la Shirikisho

  Chirwa ambaye hadi sasa amecheza mechi sita za mashindano yote Yanga bila kufunga bao hata moja, amesema kwamba anataka kucheza vizuri kuisaidia Yanga kushinda ili ajenge heshima yake.
  “Mimi kufunga itakuwa kizuri, lakini nataka zaidi kucheza vizuri kuisaidia timu kushinda, yeyote atakayefunga ni sawa kwa faida ya timu,”amesema mchezaji huyo wa Zambia.
  Chirwa bado hajazikonga nyoyo za mashabiki wa Yanga tangu amesajiliwa Julai kutokana na kutoonyesha kiwango kizuri na kukosa mabao ya wazi, ingawa anaonekana ni mchezaji mzuri.
  Baadhi ya mashabiki wa Yanga wanaonekana kumkatia tamaa, lakini wengine nafsi zao zimeridhia kumpa muda kwa sababu wanaamini ni mchezaji mzuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: CHIRWA: NIKIPANGWA OKTOBA 1, SIMBA TUTAHESHIMIANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top