• HABARI MPYA

  Jumatano, Septemba 21, 2016

  SERENGETI BOYS WAPAA KESHO WAKATI KILI QUEENS WANAWASILI NA MWALI WAO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, inatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda mjini Kigali, Rwanda kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za U-17 Afrika mwakani nchini Madagascar.
  Serengeti itakwenda Rwanda ikitoka kushinda mabao 3-2 katika mchezo wa kwanza Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, matokeo ambayo watatakiwa kwenda kuyalinda katika mchezo wa marudiano Oktoba 2.
  Mshambuliaji Yohana Oscar Nkomola aliifungia Serengeti Boys mabao mawili kipindi cha kwanza dakika ya 43 pasi ya na 45, yote kwa jitihada binafasi akifumua mashuti mazuri baada ya kuwatoka mabeki wa Kongo. 
  Kipindi cha pili, Kongo walibadilika kimchezo na kuongeza kasi ya mashambulizi langoni hadi kufanikiwa kupata bao.
  Walipata bao hilo dakika ya 71 kwa mkwaju wa penalty wa Langa-Lesse Percy uliotolewa na refa Nelson Emile Fred baada ya Mboungou Prestige kuchezewa rafu na Israel Patrick.
  Na ni wakati huo huo kipa Wa Serengeti Boys, Ramadhan Kambwili alipoumia nyama na kulazimika kutoka nafasi yake ikichukuliwa na Kevin Kayego.
  Issa Abdi Makamba aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Nkomola, aliifungia Serengeti Boys bao la tatu dakika ya 83 kwa jitihada binafasi pia akimtoka beki wa pembeni wa Kongo kushoto kabla ya kufumua shuti la kitaalamu lililotinga nyavuni. 
  Bopoumela Chardon akaifungia Kongo bao la pili dakika ya 88 akimalizia krosi ya Ntota Gedeon kutoka kushoto.
  Wakati huo huo: Mabingwa wapya wa Kombe la Chalenji la CECAFA, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania Bara maarufu kwa jina la Kilimanjaro Queens, inatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam kesho Septemba 22, 2016 saa 7.00 mchana kwa ndege ya FastJet ikitokea Mwanza.
  Mara baada ya kutua, itakwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya Coartyard iliyoko Sea View, Upanga jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata chakula cha mchana ambako watakuwako viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wale wa Serikali akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
  Timu hiyo leo Septemba 21, 2016 ilitua Kagera ambako imetumia siku ya leo kuwafariji wahanga wa tetemeko la ardhi.
  Itakumbukwa kwamba kabla ya kwenda Jinja, Uganda ambako ilivuna ubingwa huo katika fainali zilizofanyika jana kwa kuilaza Kenya katika fainali zilizofanyika Uwanja wa Njeru, Kilimanjaro Queens iliweka kambi mjini Bukoba ambako ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Burundi na kushinda mabao 3-0 Septemba 8, mwaka kwenye Uwanja wa Kaitaba.
  Kilimanjaro Queens inatarudi Kagera kusema: “Ahsante” kwa wenyeji akiwamo Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Mstafu Salum Kijuu aliyewakabidhi bendera kabla ya safari, lakini pia kuwapa pole Wahanga wa janga la Tetemeko la Ardhi wakazi lililotokea katika mikoa huo na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani. Mikoa ambayo iliathirika zaidi ni Kagera na Mwanza kadhalika nchi jirani za Uganda na Rwanda.
  Mara baada ya kuwapa pole, timu hiyo itasafiri kutoka Kagera kwa usafiri wa anga ambako taratibu za safari hiyo zitatangazwa na TFF hapo kesho ambako wananachi watapata fursa ya kuipokea na kuishangilia timu hiyo inayonolewa na Kocha Sebastina Nkoma akisaidiuwa na Edna Lema  wakiwa chini ya Mwenyekiti wa soka la wanawake, Amina Karuma.
  Safari ya ubingwa wa Kilimanjaro Queens ulianzia hatua ya makundi kwa kuilaza Rwanda manbao 3-2 kabla ya kutoka sare tasa na Ethiopia ambayo pia ilivuna ushindi wa mabao 3-2 kutoka kwa Rwanda. Tanzania na Ethiopia zilitoka sare na kurusha sarafu ambako Tanzania ikawa ya kwanza katika kundi B hivyo kucheza na Uganda ambayo ililala kwa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali. Na leo Septemba 20, 2016 ikatawazwa kuwa mabingwa kwa ushindi wa mabao 2-1.
  Timu zote shiriki zilikuwa Tanzania, Burundi, Zanzibar, Kenya, Ethiopia, Rwanda pamoja na mwenyeji Uganda. Mashindano ya Kombe la Chalenji la CECAFA kwa timu za wanawake yamefanyika kwa mara ya kwanza jambo linaloleta tafsiri kuwa michuano hiyo inaweza kuinua soka la wanawake kwa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS WAPAA KESHO WAKATI KILI QUEENS WANAWASILI NA MWALI WAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top