• HABARI MPYA

    Monday, October 13, 2014

    MALINZI NA HARAKATI ZA KURUDISHA HADHI YA SOKA YA TANZANIA, USHINDI WA STARS 4-1 DHIDI YA BENIN NI DALILI ZA MWANZO ZA MAFANIKIO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU bora ya taifa, itakayowapa raha Watanzania- hiyo ndiyo dhamira kuu ya Jamal Emil Malinzi baada ya kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akirithi nafasi ya Leodegar Chilla Tenga ambaye hakugombea baada ya kumaliza muda wake.
    Na ndiyo maana mara tu baada ya kuingia ofisini, jambo la kwanza ulikuwa mpango wa maboresho ya timu ya taifa, Taifa Stars- akiunda jopo la makocha na wachezaji wa zamani kuzunguka nchi nzima kusaka vipaji vipya. 
    Kila mkoa uliendesha mashindano maalum ya wachezaji ambao hawachezi Ligi Kuu, ili kusaka vipaji vipya na mpango uliofuata ilikuwa timu itakayopatikana ipelekwe kambini Hispania.
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi anahangaikia kuiinua tena soka ya Tanzania

    Malinzi aliamua kufanya hivyo baada ya kuona wachezaji waliopo sasa wameshindwa kabisa kuiletea mafanikio Taifa Stars, kiasi cha kufikia kufungwa nyumbani na ugenini na timu za ukanda wetu kama Uganda.
    Ukweli ni kwamba Watanzania walikuwa wamekata tamaa na Taifa Stars ya sasa na kwa kuliona hilo, Malinzi alitaka kuanza na mpango wa maboresho. Lakini vyombo vya habari viliukandia mpango huo baada ya timu kufungwa 3-0 na Burundi katika mchezo wa kirafiki Dar es Salaam.
    Sifa moja kubwa ya Malinzi ni mtu mwenye kusoma ishara za nyakati, akaamua kuirudia timu ile ile akileta kocha mpya, Mholanzi Mart Nooij- huku akifikiria namna ya kuwa na mpango wa muda mrefu wa kuwa na timu bora ya taifa.
    Viongozi wengi wa soka katika nchi hii wamekuwa hawafikirii juu ya mipango ya muda mrefu, kwa sababu labda hawataki kuja kuwanufaisha viongozi watakaoingia madarakani baada yao.
    Lakini Malinzi anatoa mfano kwa kuja na mpango wa muda mrefu, programu ya vijana inayolenga Fainali za Afrika za U17 mwaka 2019.
    Malinzi amesema katika utelezaji wa programu hiyo, wataanza na mashindano ya vijana chini ya umri chini ya miaka 12 yatakayofanyika Desemba mwaka huu mjini Mwanza, ambayo yatashirikisha kombaini za mikoa yote nchini.
    Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' kushoto akisalimiana na Nahodha wa Benin, Sessegnon Stephanie kulia kabla ya mechi jana. Benin ilikula 4-1 na cannavaro alifunga bao la kwanza   

    Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Desemba 6 hadi 12 mwaka huu, na timu zinatakiwa kuwasili Mwanza, Desemba 5 mwaka huu. Bajeti ya mashindano hayo ni Sh. Milioni 350 na Malinzi amewashukuru Wakurugenzi wa shule za Alliance (James Bwire) na Lord Baden Powell (Kanali mstaafu Idd Kipingu) kwa kukubali shule zao kuwa za kwanza kuanzia programu hiyo ya vijana.
    Pia aliishukuru kampuni ya Symbion ambayo imetoa Sh. Milioni 100 kwa ajili ya kuunga mkono mashindano hayo ya U12. Symbion ni miongoni mwa wadau wanaoshirikiana na TFF katika mpango wa miaka mitano ya programu za vijana.
    Mkurugenzi wa Symbion, Stewart John Hall aliwaonyesha Waandishi wa habari programu hiyo. 
    Lakini wakati huo huo- uboreshaji wa timu ya sasa ya taifa, kwa kuhakikisha inapata mechi katika kila kalenda ya FIFA zinaendelea na jana ilicheza dhidi ya Benin na kushinda 4-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, tena ikionyesha kiwango safi kabisa.
    Wakati Tanzania inashika nafasi ya 115 katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Benin ipo nafasi ya 78 na ilishiriki mara mbili mfululizo Fainali za Mataifa ya Afrika 2008 na 2010 kabla ya kuzikosa Fainali zilizofuata, wakati kikosi chake kimesheheni nyota wa Ulaya.  
    Kikosi cha Benin kilichokuja kucheza na Stars kinaundwa na Stephane Sessegnon (West Bromwich Albion, Uingereza), Didier Sossa (USS Krake, Benin), Abdel Fadel Suanon (Etoile Sportive du Sahel, Tunisia), Jodel Dossou (Red Bull Salzburg, Austria), Sessi D’almeida (FC Girondis Bordeaux, Ufaransa), Mohamed Aoudou (JS Saoura, Algeria) na Saturnin Allagbe (Niort, Ufaransa).
    Steve Mounie (Montpellier, Ufaransa), Farnolle Fabien (Clermont Foot Auvergne 63, Ufaransa), Jordan Adeoti (Caen, Ufaransa), Michael Pote (Omonia Nikosia, Cyprus), David Djigla (FC Girondis Bordeaux, Ufaransa) na Seidou Baraze (Kawkab Marrakech, Morocco).
    Jean Ogouchi, Centre Mberie Sportif Club, Gabon), Nafiou Badarou (ASO Chlef, Algeria), Eric Tossavi (Avrankou Omnisport, Benin), Fortune Ore (USS Krake, Benin) na Seibou Mama (Aspac, Benin).
    Mashabiki wakifurahia ushindi wa Taifa Stars jana 

    Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilikuwa ina wachezaji watatu wanaocheza nje, Juma Luizio wa ZESCO United ya Zambia, Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya DRC na Mwinyi Kazimoto wa Al Markhiya ya Qatar, wengine wote wanacheza Ligi Kuu ya Vodacom hapa nyumbani.
    Malinzi ana dhamira ya kweli ya kuleta mafanikio katika soka ya Tanzania na jitihada zake zinaonekana na ushindi wa 4-1 dhidi ya Benin ni dalili za mwanzo za mageuzi. 
    Wapinga maendeleo wapo dunia nzima, si ajabu hapa Tanzania wakatokea watu ambao hawaitakii mema soka ya nchi hii na kila kukicha wanapambana na jitihada za TFF ya Malinzi.
    Hakuna hata sababu ya Malinzi au Mjumbe yeyote wa Kamati ya Utendaji ya TFF kupoteza muda kujibizana na hao watu, bali wabakie kwenye mipango na mikakati yao ya kuleta mabadiliko katika soka ya nchi hii.
    TFF ya Malinzi iko bize na shughuli na kimaendeleo tu kwa ajili ya soka ya nchi hii, ndiyo maana jana Benin kala 4-1 na programu ya U17 mwaka 2019 imeanza kufanyiwa kazi chini ya sapoti ya Watanzania wazalendo kwa rangi na nafsi, akiwemo Luteni Mstaafu Iddi Kipingu. 
    TFF ya Malinzi iko imara kuhakikisha inakata kiu ya Watanzania, kuirejesha Taifa Stars katika fainali za michuano mikubwa. Kazi inafanyika, na inaonekana inafanyika. Hongera Malinzi, hivyo ndivyo Watanzania wanataka.
    Mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu (katikati) akipongezwa na wenzake jana baada ya kufunga katika ushindi wa 4-1
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI NA HARAKATI ZA KURUDISHA HADHI YA SOKA YA TANZANIA, USHINDI WA STARS 4-1 DHIDI YA BENIN NI DALILI ZA MWANZO ZA MAFANIKIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top