• HABARI MPYA

    Monday, February 03, 2014

    YANGA YAAMUA BAGAMOYO NDIYO MASKANI

    Na Prince Akbar, Dar es Salaam
    KIKOSI cha mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga kinarejea tena kambini  mjini Bagomoyo, Pwani kesho asabuhi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza ya mashindano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya timu ya Komorozine de Domoni kutoka Comoro itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jijini Dar es Salaam leo mchana, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema kuwa baada ya mechi ya jana waliyoshinda 1-0 dhidi ya timu ngumu ya Mbeya City, wachezaji wao walipewa mapumziko ya siku moja kabla ya kuendelea na kambi hiyo ambayo ilianza Alhamisi baada ya Yanga kutoka suluhu na mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga Jumatano.

    "Timu itakuwa kambini mjini Bagamoyo kabla ya kucheza mechi yetu ya Jumamosi," amesema Kizunguto huku akibainisha kuwa kocha wao Mholanzi Hans van Der Pluijm amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa  kufuata maagizo yake na kupata ushindi katika mechi ya juzi ambao umeifanya timu yao kukaa nafasi ya pili katika msimamo na kuwaacha Mbeya City kwa tofauti ya pointi nne wakiwa nafasi ya tatu.
    Yanga imepangwa kuanza na timu hiyo 'kibonde' katika hatua ya awali ya mashindano hayo makubwa ya klabu barani Afrika na ikifuzu mtihani huo awali, itapambana na Al Ahly ya Misri mechi ambayo tayari uongozi wa Wanajangwani umeshauza haki za matangazo ya televisheni kwa dola za Marekani 55,000 (takriban Sh. milioni 90).
    Kikosi cha Jangwani kimekuwa na utaratibu wa kuweka kambi mjini Bagamoyo kabla ya kucheza na watani wao wa jadi, Simba lakini katika siku za karibuni kimekuwa kikifanya hivyo kabla ya kumenyana na Azam FC na wageni wa ligu kuu Mbeya City ambao wanakuja juu katika anga la soka nchini.
    Azam FC, ambao wanaingia kambini leo jijini Dar es Salaam, wataanzia nyumbani pia dhidi ya Ferroviario Da Beira ya Msumbiji katika Raundi ya Awali ya Kombe la Shirikisho baranik Afrika na wakifanikiwa kuitoa Ferroviario watamenyana na mshindi kati ya St. Michel ya Shelisheli na ASSM Elgeco Plus ya Madagacar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAAMUA BAGAMOYO NDIYO MASKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top