• HABARI MPYA

    Sunday, February 09, 2014

    KWA SOKA ILE, YANGA WATATIA AIBU KWA AL AHLY

    YANGA SC jana imeanza vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Komorozine ya Comoro katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali.
    Matokeo hayo yanaiweka timu hiyo ya Jangwani katika nafasi nzuri ya kusonga mbele na kulingana na hali halisi ya wapinzani wao, unaweza kusema Yanga imekwishasonga mbele, kwani ni miujiza pekee ndiyo itakayobadilisha matokeo katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo nchini Comoro. 

    Pamoja na ushindi wa jana, bado kiwango cha uchezaji cha timu ya Yanga hakiridhishi na zaidi ushindi huo ulitokana na udhaifu wa wapinzani wao. Hali hii inajitokeza wakati tayari uongozi wa Yanga umekwishatumia fedha nyingi kutengeneza timu, kwanza kusajili wachezaji wazuri, kambi ya wiki mbili Uturuki na baadaye Bagamoyo.
    Wachezaji wa Yanga wanalipwa vizuri, wanaishi katika mazingira mazuri ambayo yanawapa fursa nzuri ya kucheza vizuri. Ukweli ni kwamba, Yanga SC wanacheza soka ya kawaida mno ambayo zaidi inatokana na uwezo wa wachezaji wenyewe.
    Hii inamaanisha kwamba timu hiyo ina makocha wa kawaida sana, wa kuongoza mazoezi tu, wasioweza kufundisha kitu ili timu icheze soka ya kuvutia.
    Yanga haina vitu vya ziada vya kiufundi, hata wakipiga pasi za visigino ni za kawaida sana kama wachezaji waliokutana kutoka timu tofauti na kuamua kucheza pamoja dhidi ya timu nyingine. Nisemeje, Yanga hawajui kudanganya zaidi ya David Luhende na Simon Msuva ambao hujirusha kuomba mipira ya adhabu na si ndani ya boksi.
    Nimebahatika kumuona kocha Msaidizi wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa akicheza soka wakati wake katika klabu hiyo na timu ya taifa, napozungumzia ufundi, bila shaka yeye ni mfano, kwani huyo jamaa alikuwa mtaaalmu mno katika eneo la kati la Uwanja. Alikuwa ana vitu.
    Yanga inashambulia kupitia pembeni na staili ni moja tu, mipira mirefu inapigwa pembeni, mawinga wanakimbiza wanapiga krosi ili washambuliaji waunganishe.
    Inapokutana na timu yenye safu ya ulinzi imara yenye uwezo wa kuokoa krosi, tumekuwa tukijionea inapata ushindi wa tabu sana. Katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, hadi sasa Yanga haijashinda japo mabao matatu katika mechi moja.
    Mbaya zaidi hata safu ya ulinzi ya Yanga bado ni ugonjwa wa moyo na katika hili tatizo si wachezaji, au mchezaji fulani bali safu ya ulinzi haina mfumo mzuri wa ukabaji au uchezaji kwa jumla na ndiyo maana jana hata Wacomoro walifika langoni kwao na kuwajaribu.
    Yote haya yanarudi katika benchi la ufundi, bado halijafanya kazi yake vizuri. Sina shaka na Charles Boniface Mkwasa, huyo ni kocha mzuri na mtaalamu, ila sina imani na bosi wake Hans van der Pluijm kama ni mwalimu mzuri, kwa sababu hata rekodi yake huko alikotoka si nzuri.
    Sasa tatizo nini? Mkwasa hapewi nafasi ya kuingiza falsafa zake za uchezaji ndani ya timu, au? Labda, maana yake hata kwenye mechi mtu ambaye husimama kuzungumza na wachezaji ni huyo babu wa Uholanzi, maana yake anawakumbusha wachezaji alichowafundisha. 
    Sasa anawafundisha nini ikiwa wachezaji hawawezi hata kutumia mipira iliyokufa kutengeneza nafasi za kufunga, wanakabika kwa urahisi, wanapitika kwa urahisi, wanaingia kwa urahisi kwenye mitego ya kuotea, wao hawawezi kutega mitego ya kuotea kwa wapinzani. 
    Haruna Niyonzima ni fundi sana, katika mfumo bora anatakiwa kutumika kama ambavyo Simba SC wanamtumia Amri Kiemba, wakati huo huo wanakuwapo viungo wawili kama kawaida katikati, wa chini na juu na huko mbele unakuwapo muundo fulani wa wachezaji watatu kukamilisha safu ya ushambuliaji. Wazi Yanga itafurahisha wapenzi wake.
    Nawapongeza Yanga SC kwa ushindi wao wa jana, lakini waelewe kwamba bado timu yao haichezi soka ya kufurahisha na kama hawatabadilika, wakirudi kutoka Comoro watapanda ndege ya mwisho kwenda Cairo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA SOKA ILE, YANGA WATATIA AIBU KWA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top