• HABARI MPYA

    Thursday, February 06, 2014

    IVO MAPUNDA AWAOMBA RADHI SIMBA SC, ASEMA…

    Na Mahmoud Zubeiry, Morogoro
    KIPA namba moja wa klabu ya Simba SC, Ivon Philip Mapunda amewaomba radhi wapenzi wa Simba SC kwa kufungwa bao jepesi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, timu hizo zikitoka sare ya 1-1.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana baada ya mechi hiyo, Ivo alisema kwamba anajisikia vibaya sana kila anapolikumbuka bao lile, lakini hana jinsi zaidi ya kukubaliana na hali halisi.
    Ivo Mapunda kushoto akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kabla ya mchezo wa jana


    “Kuna vitu viwili, kwanza lile eneo nililuwa nimesimama lina utelezi na mpira ulipoteza mwelekeo kwa sababu ya upepo, nilijitahidi lakini bahati mbaya ikawa vile, kwa kweli naomba sana wapenzi na wanachama wa Simba waniwie radhi,”alisema Ivo.
    Ivo jana alifungwa bao la kwanza katika Ligi Kuu tangu aanze kuichezea Simba SC na la tatu kwa ujumla kwenye mashindano yote aliyocheza na jezi ya Wekundu wa Msimbazi, mengine katika ushindi wa 3-1 dhidi ya mahasimu, Yanga Desemba 21, mwaka jana mechi ya Nani Mtani Jembe na Januari 13, mwaka huu katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi.  
    Simba SC jana ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar iliyomaliza pungufu ya mchezaji mmoja baada ya Nahodha wake, Shaaban Nditi kuonyeshwa kadi nyekundu kipindi cha pili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
    Hadi mapumziko tayari Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi dakika ya nane.
    Mgosi alifanyiwa madhambi na beki Donald Mosoti upande wa kulia wa Uwanja, lakini akainuka na kuendelea kukimbia na mpira na refa akaridhia.
    Akapiga mpira unaofanana na krosi ambao ulielekea kwenye himaya ya kipa Ivo Mapunda, lakini kwa bahati mbaya mpira ukamteleza kipa huyo na pamoja na jitihada za kutaka kuurejesha mikononi mwake, ukadondokea  nyavuni.  
    Simba SC ilipigana kuanzia dakika ya tisa kutaka kusawazisha bao hilo, lakini hawakufanikiwa hadi zilipotimia dakika 45 za kipindi cha kwanza.
    Kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic alimtoa nje kiungo Awadh Juma Issa dakika ya 36 akamuingiza mshambuliaji Ali Badu Ali na kidogo safu ya ushambuliaji ilichangamka.
    Kipindi cha pili Simba SC ilicharuka na kufanya mashambulizi ya nguvu lango ni mwa Mtibwa, hatimaye kupata bao la kusawazisha dakika ya 50, mfungaji Mrundi Amisi Tambwe, aliyemalizia pasi ya Haroun Chanongo.  
    Mtibwa ikapata pigo dakika ya 69, baada ya Nahodha wake, Nditi kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumtolea lugha chafu refa Jeonisia Rukyaa wa Kagera.
    Matokeo hayo yanaifanya Simba SC itimize pointi 31 baada ya kucheza mechi 16 na kupanda hadi nafasi ya tatu mbele ya Mbeya City yenye pointi 31 pia, lakini Wekundu wa Msimbazi wana wastani mzuri zaidi wa mabao, 18-9.
    Yanga SC yenye pointi 35 ni ya pili na Azam FC inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 36, wakati Mtibwa Sugar inatimiza pointi 22 baada ya kucheza mechi 16 pia hivyo kubaki nafasi ya tano.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: IVO MAPUNDA AWAOMBA RADHI SIMBA SC, ASEMA… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top